Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nina jukumu la kuiambia serikali kwamba tuko hapa kusaidia kupunguza na kuondoa athari kwa raia wa hali hizi-Filippo Grandi  

Maelfu ya wakimbizi wamevuka mpaka kutoka Ethiopia kuingia Sudan wakikimbia mgogoro katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.
© WFP/Leni Kinzli
Maelfu ya wakimbizi wamevuka mpaka kutoka Ethiopia kuingia Sudan wakikimbia mgogoro katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.

Nina jukumu la kuiambia serikali kwamba tuko hapa kusaidia kupunguza na kuondoa athari kwa raia wa hali hizi-Filippo Grandi  

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi ametembelea kambi ya wakimbizi ya Mai-Aini katika mkoa wa Tigray nchini Ethiopia, na kujionea hali ilivyo na akaiahidi serikali kusaidia kupunguza madhara ya hali hiyo kwa raia.

Katika kambi ya wakimbizi ya Mai-Aini kwenye mkoa wa Tigray Ethiopia, hali ni ya msongamano, nyumba dhaifu na sura zilizokosa matumaini. Kambini hapa wapo wakimbizi wa ndani kutokana na mzozo wa Tigray. Na wako wakimbizi kutoka nchi jirani ya Eritrea. 

Kamishna wa UNHCR, Filippo Grandi akimekutana na wakimbizi kutoka Eritrea katika ziara yake hii ya siku nne nchini Ethiopia.  Kwa miezi takribani miwili, kulikuwa na usitishaji wa mgao wa misaada ya kibinadamu katika kambi za wakimbizi za Tigray kufuatia kuanza kwa mzozo katika eneo hili mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka jana 2020. Kukosekana kwa usalama kuliwalazimisha wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kujiondoa katika eneo hilo. Ukosefu wa usalama ulilazimisha wafanyikazi wa kibinadamu kujitoa kutoka eneo hilo. Kamishna Grandi anasema, "ni vyema sana kwamba vibali vimepatikana katika siku za hivi karibuni kupeleka shehena katika maghala ya Tigray, hasa huko Mekelle, nadhani hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa bidhaa hizi, shehena hii, hususani chakula, lakini pia vitu visivyo chakula, vitoke nje na kufika kwa watu wanaohitaji.” 

UNHCR, imeweza kupata tena nafasi ya kuingia katika kambi mbili za wakimbizi za Mai Aini na Adi Harush mwezi uliopita na kuwakuta wakimbizi wakiwa katika uhitaji mkubwa wa huduma. Bwana Grandi baada ya kurejea mjini Addis Ababa anasimulia alichoongea na wakimbizi akisema,"wale ambao tumeongea nao walikuwa wakitoka kwenye kambi nyingine mbili wameripoti masuala yanayotusikitisha sana. Wameripoti kwamba wamekatiwa msaada, kama tunavyojua kwa wiki kadhaa. Wengine wao walituambia na kumwambia Waziri kwamba walikuwa wameamua kula majani kwa sababu hakukuwa na chakula kingine. Waliongea pia kuhusu kukwama katika majibizano ya risasi yaliyokuwepo mwanzoni mwa operesheni za kijeshi. Wamezungumza pia juu ya kupenya kwa watu wenye silaha katika kambi hiyo, matukio ya mauaji, utekaji nyara, na pia wengine walilazimishwa kurudi Eritrea mikononi mwa vikosi vya Eritrea vilivyopo katika eneo hilo. Wengine waliripoti kwamba wakimbizi wengine wamechagua wenyewe Eritrea kutokana na ukosefu wa usalama uliopo katika eneo hilo.” 

Kaskazini zaidi mwa Tigray, UNHCR haijawa na nafasi ya kufikia kambi za wakimbizi za  Shimelba na Hitsats. Karibu wakimbizi 3000 wamewasili katika kambi za kusini kutoka kaskazini wakitafuta usalama, wakitembea kwa siku kadhaa bila chakula na wameacha kila kitu nyuma.  

Bwana Grandi anatoa wito akisema, "ni muhimu kwamba tuwasiliane tena na wakimbizi hao ambao bado wametawanywa kutoka Hitsats na Shimelba. Tunakadiria kunaweza kuwa na kati ya watu elfu 15 na 20, pengine chini kidogo, ambao bado wametawanywa katika maeneo ambayo hatuwezi kufika. Na wakati kuhamia kwenye kambi za kusini kunaendelea, nadhani kwamba tunahitaji kuharakisha operesheni hiyo. Na ili hiyo iweze kuharakishwa na kuwaleta watu kwenye usalama mbali na maeneo yasiyo salama, ni muhimu kwamba ARRA, shirika la wakimbizi la Ethiopia, kwa msaada wetu, tuweze kufikia maeneo hayo. " 

UNHCR inatoa wito wa kupewa ufikiaji zaidi ili kusaidia maelfu ya wakimbizi waliosambaa katika eneo lote. Usambazaji wa vitu visivyo vya chakula kama blanketi, taa za jua na vifaa vya nyumbani unaendelea katika kambi za kusini.