Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tigray Ethiopia, WFP yatangaza kipaumbele chake

Wakimbizi waliowasili kutoka Tigray Ethiopia wakileta msaada kwa ajili ya kukarabati makazi kambi ya Raquba, Kassal, Sudan.
UNFPA/Sufian Abdul-Mouty
Wakimbizi waliowasili kutoka Tigray Ethiopia wakileta msaada kwa ajili ya kukarabati makazi kambi ya Raquba, Kassal, Sudan.

Tigray Ethiopia, WFP yatangaza kipaumbele chake

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP limekaribisha kusainiwa kwa makubaliano ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za kibinadamu ambazo hazina kizuizi, endelevu na salama kwa maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Serikali ya Shirikisho katika mkoa wa Tigray na maeneo yanayopakana na mikoa ya Amhara na Afar. 

WFP imesema kipaumbele chake ni kuwatafuta na kuwapata wakimbizi wapatao 50,000 wa Eritrea ambao kabla ya vita walipata msaada wa chakula cha WFP katika kambi nne za Tigray. “Inawezekana baadhi ya watu hawa wanaweza kuwa wamekimbia mapigano.” Imesema sehemu ya taarifa ya WFP iliyotolewa hii leo Ijumaa mjini Geneva Uswisi.  

WFP kwa hivyo inaendelea na ushiriki wake kuhusu jinsi ya kuharakisha upelekaji wa chakula katika kambi za wakimbizi huko Tigray na pia kufikia watu walio na uhitaji mahali pengine. Pia WFP ilitoa lishe ya ziada kwa watu 42,000 katika mkoa huo na ikawasaidia watu 210,000 na msaada kwa wakulima wadogo kusaidia kujenga mnepo wao. 

Kwa jumla, watu milioni 1 walikuwa wakipokea msaada kabla ya mapigano. Kabla ya tathmini za Umoja wa Mataifa na wadau, Umoja wa Mataifa kwa muda mfupi, awali ulikadiria kuwa hadi watu milioni 2 kutoka Mkoa wa Tigray watahitaji msaada. 

“Tunatambua kuwa vurugu zinaweza kuwa zilivuruga shughuli za WFP zilizopo huko Tigray na kuzalisha idadi mpya ya watu wanaohitaji msaada.” Imesema WFP. 

WFP iko tayari kushughulikia kuongezeka kwa mzigo wa watu walio na uhitaji Tigray mara tu mahitaji yatakapotathminiwa.  

Hata hivyo, nchini Ethiopia, WFP inakabiliana na upungufu wa dola za kimarekani milioni 210 ambazo ni asilimia 67 za kusaidia watu milioni 6.2 kote nchini kufikia Mei 2021.