Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa sasa hakuna njia ya kufikisha misaada ya kibinadamu Tigray Ethipia:OCHA 

Eneo la Tigray linakabiliwa na changamoto nyingi za kimaendeleao nchini Ethiopia
© UNICEF/Zerihun Sewunet
Eneo la Tigray linakabiliwa na changamoto nyingi za kimaendeleao nchini Ethiopia

Kwa sasa hakuna njia ya kufikisha misaada ya kibinadamu Tigray Ethipia:OCHA 

Amani na Usalama

Shirika la la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya dharura na misaada ya kibinadamu OCHA leo limeonya kwamba kwati huu ambapo mawasiliano ya simu yamekatwa na njia za usafiri kuvurugwa katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia ni vigumu kufikisha misaada muhimu ya kibinadamu inayohitajika au kutathimini hali ya kibinadamu. 

Shirika hilo limeongeza kuwa “Barabara zikiwa zimefungwa chakula, huduma za afya na misaada mingine ya dharura haina njia yoyote ya kufika Tigray, kuandaa misaada hiyo au kuongeza iliyopungua , haiwezekani. Mawasiliano ya simu bado yamekatwa na kufanya ufikishaji taarifa na kuhakiki ripoti za vyombo vya Habari kuwa vigumu sana kwa jumuiya ya watoa misaada ya kibinadamu lakini pia kufuatilia watu wanakokwenda na mahitaji mengine ya kibinadamu.” 

OCHA imesema mbali yay a kukosa mawasiliano ya aina yoyote huduma za benki pia zimearifiwa kufungwa na mafgari kupigwa marufuku kuwa barabarani ndani nan je ya jimbo hilo. 

Tayari kuna upungufu wa bidhaa muhimu hali ambayo inawaathiri zaidi watu walio hatarini. 

Machafuko yalizuka jimboni Tigray wiki iliyopita yakihusisha vikosi vya serikali na vya eneo hilo kufuatia ripoti za kushikiliwa kwa kambi ya jeshi katika mji mkuu wa Tigray , Makelle baada ya waziri mkuu kutoa amri ya mashambulizi ya kijeshi. 

Katika taarifa iliyotolewa wakati huo Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa “Kuchukuliwa hatua mara moja kusitisha mvutano na kuhakikisha suluhu ya amani ya mzozo huo inapatikana.” 

Familia wakichota maji katika kisima kinachofadhiliwa na UNICWF katika eneo la Kilte Awlalo, TIgray nchini Ethiopia.
© UNICEF/Zerihun Sewunet
Familia wakichota maji katika kisima kinachofadhiliwa na UNICWF katika eneo la Kilte Awlalo, TIgray nchini Ethiopia.

Hofu kubwa kwa raia 

OCHA pia imeelezea hofu yake kuhusu ulinzi kwa raia hususan Watoto, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu wakati huu wa machafuko. 

“Hatari zilizopo za ulinzi kwa Watoto zinauwezekano wa kuongezwa na machafuko haya” imeongeza OCHA huku ikisisitiza kwamba hatari kubwa zaidi ipo kwa Watoto waliotenganishwa na wazazi au walezi wao, ambapo wanaweza kutukizwa katika unyanyasi na ukatili. 

Pia kuna hofu kuhusu uharibifu wa mazao uliosababishwa na nzige wa jangwani, hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula na kusambaa kwa COVID-19

Tutaendelea kutoa usaidizi 

OCHA imerejea kusema kwamba Umoja wa Mataifa na mashirika wadau wamejizatiti kuendelea kuwepo Ethiopia na kufikisha msaada wa kibinadamu unaohitajika na kwamba mpango wa usaidizi kwa ajili ya jimbo la Tigray unaandaliwa haraka. 

Kwa mujibu wa shirika hilo kuna watu 600,000 wanaopokea msaada wa chakula katika jimbo hilo ambapo kati yao 100,000 ni wakimbizi wa ndani na takribani 96,000 ni wakimbizi.