Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunapopambana na COVID-19 tusiyape kisogo maradhi kama TB:WHO

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nembo ya kutokomeza Kifua Kikuu ikiwa imewekwa.
UN News/Daniel Dickinson
Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nembo ya kutokomeza Kifua Kikuu ikiwa imewekwa.

Tunapopambana na COVID-19 tusiyape kisogo maradhi kama TB:WHO

Afya

Tunapopambana na janga la kimataifa la afya COVID-19 ni wakati pia wa kutafakari na kutoyapa kisogo maradhi mengine makubwa ikiwemo kifua kikuu au TB, amesema mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO.

Mkurugenzi huyo Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus ameikumbusha dunia na kila mtu kwamba ingawa virusi vya corona, COVID-19 ndio vinavyogonga vichwa vya habari kila kona ya dunia  hivi sasa lakini kuna gonjwa lingine la mfumo wa hewa ambalo ni chagamoto kwa dunia“Kuna ugonjwa mwingine wa mfumo wa hewa ambao unazuilika na kutibika lakini unakatili maisha ya watu milioni 1.5 kila mwaka na gonjwa hilo la muda mrefu ni kifua kikuu.”

Ameongeza kuwa wakati dunia leo ikiadhimisha siku ya kifua kikuu ambayo kila mwaka hua Machi 24, hii ni fursa ya kuwakumbusha viongozi wa dunia kuhusu wajibu wao na ahadi waliyoiweka ya kutokomeza madhila na vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huu mbaya na wa muda mrefu wa TB.

“Dunia inachukua hatua muafaka na za haraka kukabiliana na COVID-19, tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kukumbatia lengo na uharaka huo kwa vita dhidi ya kifua kikuu ili kuwa na dunia yenye afya, salama na ya usawa kwa kila mtu.”

Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa
Photo: The Global Fund/John Rae
Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa

Kaulimbiu ya siku ya mwaka huu ni “wakati umewadia kutokomeza TB” na tawkimu za WHO zinaonyesha kwamba kifua kikuu au TB ni ugonjwa wa kuambukiza unaokatili maisha ya watu wengi zaidi duniani.

Kila siku zaidi ya watu 4,000 wanakufa kutokana na TB na wengine zaidi ya 30,000 wanaugua ugonjwa huu ambao unazuilika na kutibika.

Na katika kuhakikisha gonjwa hili linatokomezwa WHO imetangaza muongozo mpya kuhusu matibabu ya kifua kikuu ambao utasaidia kuwa na matokeo mazuri ya tiba kwa wagonjwa na kuokoa maisha.

Tangu mwaka 2,000 WHO inasema juhudi za kimataifa za kukabiliana na kifua kikuu zimeokoa maisha ya watu milioni 58.