Tuwekeze kwenye tafiti na matibabu ya TB kunusuru kizazi cha sasa na kijacho - WHO

Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa
Photo: The Global Fund/John Rae
Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa

Tuwekeze kwenye tafiti na matibabu ya TB kunusuru kizazi cha sasa na kijacho - WHO

Afya

Ikiwa leo ni Siku ya kifua kikuu duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO limetoa wito kwa serikali na wadau kuongeza uwekezaji katika huduma za Kifua Kikuu na utafiti hususan kwa watoto na vijana. 

WHO inasema kuwa ugonjwa wa Kifua Kikuu au TB, ulishughulikiwa ipasavyo duniani kote na kwamba maisha ya watu milioni 66 yaliokolewa.

Lakini janga la COVID-19 limebadilisha mafanikio hayo kwa kuwa rasilimali nyingi ziliwekezwa katika kupambana na janga hilo na kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja, vifo vya TB viliongezeka mwaka wa 2020.

Wito wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus katika siku hii ya TB duniani ni kwa nchi na wafadhili kuongeza matumizi katika uchunguzi, matibabu na kinga ya TB akitolea mfano mwaka 2020, ufadhili ulikuwa chini ya nusu ya lengo la kimataifa la dola bilioni 13 kila mwaka ifikapo 2022.

Tweet URL

Dkt.Tedros amesema “uwekezaji wa haraka unahitajika ili kukuza na kupanua ufikiaji wa huduma na zana za ubunifu zaidi za kuzuia, kugundua na kutibu TB ambayo inaweza kuokoa mamilioni ya maisha kila mwaka, ukosefu wa usawa na kuepusha hasara kubwa za kiuchumi.”

Ufadhili wahitajika zaidi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa WHO anayehusika na mipango ya  kifua kikuu Dkt. Tereza Kasaeva amesema ili kunusuru kizazi cha sasa na kijacho ni vyema suala la ufadhili likashughulikuwa kwa haraka na WHO imetoa miongozo mipya ya namna ya kuwasaidaia.

Mtoto akipokea dawa za TB nchini Sudan Kusini kwa msaada wa Global Fund kupambana na VVU,TB na Malaria
Mtoto akipokea dawa za TB nchini Sudan Kusini kwa msaada wa Global Fund kupambana na VVU,TB na Malaria, by UNDP South Sudan/Brian Sokol

Anasema watoto na vijana walio na TB wako nyuma kuliko watu wazima katika kupata kinga na matibabu,  miongozo ya WHO iliyotolewa leo ni mabadiliko kwa watoto na vijana ili kuwasaidia kugunduliwa na kupata huduma mapema, na kusababisha matokeo bora na kupunguza maambukizi. Kipaumbele sasa ni kupanua haraka utekelezaji wa mwongozo katika nchi nzote iili kuokoa maisha ya vijana na kuepusha mateso.

Akinukuu ripoti ya mwaka 2020 ya TB Dkt. Kasaeva amesema, imekaridia asilimia 63 ya watoto na vijana chini ya miaka 15 wenye Kifua Kikuu hawakufikiwa na matibabu ya kuokoa maisha yao au taarifa zao hazijawasilishwa na kwa upande wa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano hali ni mbaya zaidi kwa kuwa asilimia 72 hawajafikiwa na matibabu.

WHO imeeleza takriban theluthi mbili ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 waliohitimu hawakupata kinga ya kuzuia TB na hivyo kundi  hilo lipo katika hatari ya kupata ugonjwa huo.