Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Surua inaendelea kusambaa kwa kasi duniani:WHO

Chanjo ya kupambana na mlipuko wa surua inafanyika katika kambi hii ya wakimbizi wa ndani ya Bunia nchini Congo DRC, (Julai 2019)
© UNICEF/Marixie Mercado
Chanjo ya kupambana na mlipuko wa surua inafanyika katika kambi hii ya wakimbizi wa ndani ya Bunia nchini Congo DRC, (Julai 2019)

Surua inaendelea kusambaa kwa kasi duniani:WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema kwamba mlipuko wa surau unasambaa kwa kasi duniani kote na kuyaweka maisha ya mamilioni ya watu hatarini.

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa mapema leo inasema miezi sita ya mwanzo yam waka huu 2019 , idadi ya visa vya surau vilivyoripotiwa iko juu sana ikilinganishwa na mwaka 2016, na kwamba mlipuko wa surua umeleta shinikizo kubwa katika mifumo ya afya na kusababisha magonjwa, ulemavu na vifo.

WHO ukilinganisha na wakati kama huu mwaka jana mwaka huu visa vilivyoripotiwa ni mara tatu zaidi na nchi zilizotajwa kuwa na idadi kubwa ya visa mwaka huu ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Madagascar na Ukraine.

Hata hivyo WHO inasema visa Madagascar vimepungua kwa kiasi kikubwa kufuatia kampeni ya dharura ya chanjo iliyofanyika nchi nzima.

Hivi sasa milipuko mikubwa ya surua inaendelea nchini Angola, Cameroon, Chad, Kazakhstan, Nigeria, Ufilipino, Sudan Kusini, Sudan na Thailand. Marekani matahalani imeripoti idadi kubwa ya visa vya surua kuwahi kushuhudiwa kwa miaka 25.

Shirika hilo la afya duniani limesema milipuko mikubwa ya surua iko katika nchi zenye kiwango kidogo cha utoaji chanjo  hivi sasa au siku za nyuma, hali ambayo imewaacha mamilioni ya watu katika hatari ya kupata ugonjwa huo.

Wakati huohuo WHO imesema milipuko ya muda mrefu inatokeo hata katika nchi zenye kiwango kikubwa cha chanjo kitaifa kutokana na kutokuwepo kwa usawa katika utoaji chanjo hiyo, mapengo miongoni mwa jamii, maeneo waliko watu  na miongoni mwa rika fulani.

Shirika hilo limeonya kwamba kunapokuwa na idadi kubwa ya watu ambao hawajapatiwa chanjo na kukumbwa na surua basi inaweza kusambaa haraka sana.

WHO imemtaka kila mmoja kuhakikisha chanjo zao zinakwenda na wakati, kwani dozi mbili zinahitajika ili kumlinda mtu dhidi ya ugonjwa wa surua na kuhakikisha wanathibitisha hali yao ya chanjo kabla ya kusafiri.