Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya Polio, Surua na Rubela zawasili Libya kuokoa watoto-UNICEF

Chanjo
UNICEF/UN060405/Llaurado
Chanjo

Chanjo dhidi ya Polio, Surua na Rubela zawasili Libya kuokoa watoto-UNICEF

Afya

Shehena ya dozi milioni 4.7 ya dawa za  chanjo dhidi ya surua, polio na rubella imewasili Libya ambapo chanjo hizo zitapatiwa watoto kwenye kampeni itakayoanza mwishoni mwa mwezi ujao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF limekodi ndege maalum kusafirisha chanjo hizo pamoja na dozi zingine milioni 2.75 za matone ya vitamini A ambayo pia itatolewa kwa watoto.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo huko Tripoli, Libya vifaa vingine vilivyomo kwenye shehena hizo ni pamoja na sindano na ambapo walengwa kwa kampeni hiyo ya chanjo itakayoendeshwa kwa ushirikiano na shirika la afya ulimwenguni, WHO na lile la wahamiaji, IOM ni watoto milioni 2.75.

Mwakilishi maalum wa UNICEF nchini Libya, Abdel-Rahman Ghandour, amesema kuwa ugonjwa hatari kama vile surua haubagui na unaweza kumshambulia mtoto yeyote yule.

Ameongeza kuwa “tunashirikiana kwa karibu na mamlaka za Libya  kuhakikisha kuwa chanjo inapatikana kote nchini hata na maeneo ambayo ni vigumu kuyafikia, kwani kila mtoto ana haki ya kupewa chanjo.”

 Mgogoro unaoendelea kwa sasa nchini Libya umevuruga karibu miundombinu yote ya utoaji wa huduma za kiafya na uwekezaji mdogo katika sekta ya afya  nao pia umeathiri sana mipango kadhaa muhimu pamoja na ya kuwapa chanjo watoto.

Hali hiyo inazidi kutatizika kutokana na hali ya wahamiaji wanaohaha kwenda Ulaya wakitumia njia ya Libya, wengi wao  huwa hawapati chanjo nchini mwao wanakotoka ama hukosa dozi zinazohitajika nchini Libya, kwani chanjo za kila mara hazitoshi nchini humo.

UNICEF, WHO pamoja na fuko la Umoja wa Mataifa linalohusika na  masuala ya dharura CERF wametenga  dola za kimarekani milioni 5 zisaidie kuendesha zoezi la kutoa chanjo kwa watoto dhidi ya Surua, Polio pamoja na kutoa matone ya Vitamin A.