Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni dhidi ya polio na Surua yaanza leo Sudan ikilenga zaidi ya watoto milioni 11.

Chanjo ya polio
UN
Chanjo ya polio

Kampeni dhidi ya polio na Surua yaanza leo Sudan ikilenga zaidi ya watoto milioni 11.

Afya

Shirika la la Afya duniani WHO kwa kushirikiana na Wizara ya afya ya Sudan, fuko la chanjo duniani, GAVI na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, hii leo wamezindua kampeni kubwa ya chanjo dhidi ya surua na polio nchini Sudan kwa zaidi ya watoto milioni 11 wa kuanzia umri wa mwezi 0 hadi miaka 10.

Taarifa iliyotolewa na WHO hii leo mjini Khartoum inasema chanjo hiyo itaambatana na utoaji wa matone ya vitamini A na itatolewa kuanzia leo hadi tarehe pili mwezi ujao wa Mei.

Takwimu rasmi nchini Sudan zinaonesha kuwa surua ni ugonjwa wa tatu kwa kusababisha vifo kwa watoto wachanga na ni ugonjwa wa kwanza miongoni mwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu wa 2019, visa 834 viliripotiwa ikilinganishwa na visa 4980 kwa mwaka mzima wa 2018.

Ingawa programu za chanjo ya polio na surua ziko tofauti, safari hii zimeletwa pamoja ili kuleta uhakika wa afya na kufikia matokeo ya afya yanayokusudiwa nchini Sudan. 

WHO inasema zaidi ya wafanyakazi wenye ujuzi mkubwa wapatao 38,826 wa chanjo, wahudumu wa afya na wahamasishaji wa jamii wamekusanywa ili kufanya kampeni hii kubwa.

Waziri wa afya wa Sudan Dkt Al-Saddig Mahjoub Al Faki Hashem akizungumzia mpango huo wa chanjo amesema, “juhudi zetu za pamoja zimeleta tofauti kubwa katika programu ya chanjo ya surau na polio nchini kote. Majimbo yote 18 yamefikiwa yakiwa na jumla ya maeneo 189.”

Naye Dkt Naeema Al Gasseer, mwakilishi wa WHO ncihni Sudan anasema, “kampeni hii kubwa ya chanjo ni shughuli muhimu katika kazi inayoendelea Sudan kuwalinda watu wote dhidi ya magonjwa yanazuilika kwa chanjo. Tutaendelea na jitihada zetu kufikia lengo hili na kuhakikisha Sudan isiyo na polio na surua.”

Kampeni hii ya pamoja ya chanjo dhidi ya polio na surua ni ya kwanza nchi nzima tangu mwaka 2014. Imepunguza pia gharama za uratibu wa chanjo kwa njia ya matone kwa mtoto kutoka dola 0.61 hadi dola 0.11, ambacho ni kiwango kidogo kuwahi kurekodiwa katika programu za chanjo nchini Sudan.