Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

"Ajabu na kweli," surua yashamiri hata kwenye nchi zinazoongoza kwa kutoa chanjo- WHO

Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya surua nchini Paraguay
Picha:WHO/PAHO
Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya surua nchini Paraguay

"Ajabu na kweli," surua yashamiri hata kwenye nchi zinazoongoza kwa kutoa chanjo- WHO

Afya

Visa vya surua vimeendelea kuongezeka mwaka 2019 huku takwimu za mapema zikionyesha kwamba visa vilivyoripotiwa viliongezeka kwa asilimia 300 katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu wa 2019 ikilinganishwa na kipindi hicho mwaka 2018.

Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, licha ya kwamba takwimu hizo ni za muda lakini mweleko ni dhahiri.

“Nchi nyingi ziko katikati ya mlipuko mkubwa wa surua katika kanda zote za dunia zikishuhudia ongezeko la visa ikiwemo milipuko inayoshuhudiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Georgia, Kazakhstan, Krygyzstan, Madagascar, Myanmar, Ufilipino, Sudan, Thailand, Ukraine na kusababisha vifo vya watu wengi ikiwemo watoto,” imesema WHO.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni ongezeko la visa vya surua vimetokea pia katika nchi ambako kuna idadi kubwa ya watu waliopatiwa chanjo dhidi ya surua, ikiwemo Marekani, Israeli, Thailand na Tunisia wakati ugonjwa ukisambaa kwa idadi kubwa ya watu wasio na kinga.

Surua ni moja ya magonjwa yanayombukizwa zaidi, ukiwa na hatari ya maambukizi ya juu. Takwimu za mwaka 2017 zinaonyesha idadi ya vifo 110,000.

Aidha hata katika nchi za kipato cha juu, changamoto kutokana na surua takriban robo ya visa vyote huishia hosptalini huku kukiwa na uwezekano wa ulemavu wa muda mrefu, uharibifu wa ubongo na ulemavu wa kutoona na kusikia.

WHO inasema kwamba surua inazuilika kupitia dozi mbili za chanjo, hata hivyo kwa muda wa miaka kadhaa uwasilishaji wa chanjo kimataifa wa dozi ya kwanza ya surua umesalia asilimia 85 ikiwa ni upungufu wa asilimia 95 inayohitajika kwa ajili ya kuzuia milipuko na hiyo inawaacha watu wengi na jamii katika hatari. Dozi ya pili licha ya ongezeko inafikia asilimia 67 tu ya watu.

Mathalani, serikali, wadau,  mkakati dhidi ya surua na Rubella, fuko la chanjo duniani, GAVI, Shirikla la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wameainisha operesheni za kukabiliana na milipuko katika nchi mbali mbali na kuimarisha huduma za afya na uwasilishaji wa chanjo.

 Mafanikio baada ya hatua

Baada ya kampeni ya dharura ikilenga watoto milioni saba wa umri wa kati ya miezi sita hadi miaka tisa, nchini Madagascar sasa wanashuhudia kupungua kwa visa vya surua na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

Nako Ufilipino, takriban dozi 3 890 000 za surua na rubella zimetolewa kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kunatarajiwa uzinduzi wa chanjo ya pamoja ya surua na polio.

Kwa ushirikiano wa mamlaka za mitaa, WHO na UNICEF waliendesha kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya surua na polio nchini Yemen na kufikia watoto milioni 11.6 ikiwa ni asilimia 90 ya watoto wa kati ya umri wa miezi sita hadi miaka 16 nchini kote.