Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 5 wanyongwa Iran na Saudi Arabia,  UNICEF yapaza sauti

Bendera ya Iran (Kati) ikipepea kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani
UN /Loey Felipe
Bendera ya Iran (Kati) ikipepea kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani

Watoto 5 wanyongwa Iran na Saudi Arabia,  UNICEF yapaza sauti

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya ripoti za mara kwa mara za kuuawa kwa watoto kwenye mataifa ya kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, MENA.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo huko Amman nchini  Jordan imenukuu ripoti za hivi karibuni zaidi za kunyongwa kwa watoto watano kwenye matukio mawili tofauti nchini Iran na Saudi Arabia, visa vilivyofanyika wiki mbili zilizopita.

Ripoti zinasema huko Iran, wavulana wawili wenye umri wa miaka 17 walinyongwa gerezani ambako walikuwa wanashikiliwa huko Shiraz, kusini mwa nchi hiyo.

Familia za watoto hao wawili yaelezwa kuwa hazikuwa zimepatiwa taarifa za awali kuhusu adhabu dhidi ya watoto wao.

bendera ya Saudi Arabia ikipepea makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York
UN Photo/Loey Felipe
bendera ya Saudi Arabia ikipepea makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York

Huko Saudi Arabia, ripoti zinasema watoto watatu waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo yadaiwa walinyongwa hadi kufa tarehe 23 mwezi uliopita wa Aprili.

“Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto kama ilivyoidhinishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imenukuu kifungu kinachosema ya kwamba, “hakuna mtoto anayepaswa kuteswa au kufanyiwa ukatili wowote, au kutendewa kinyume na ubinadamu au kuadhibitiwa. Hakuna adhabu ya kifo au kifungo cha maisha bila fursa yoyote ya kuachiwa huru inapaswa kuhukumiwa mtu yeyote mwenye  umri wa chini ya miaka 18. Iwapo atapatikana na hatia ya kuvunja sheria, mtoto anapaswa kutendewa kwa ut una kwa njia ambayo itazingatia mahitaji ya umri wake. Wana haki ya msaada wa kisheria na uendeshaji wa kesi ufanyike kwa haki.”


UNICEF imesema wakati huu ambapo dunia inaadhimisha miaka 30 tangu kupitishwa kwa CRC, shirika hilo linaendelea kusisitiza umuhimu wa nchi zilizotia saini mkataba huo zizingatie misingi yake kuhusiana na uwekaji watoto rumande, hukumu na adhabu ya kifo.

Shirika hilo limesema liko tayari kusaidia serikali na taasisi za mahakama katika kuendeleza na kuanzisha mifumo mbadala ya kusweka watoto rumande.