Watoto hatarini Syria na Yemen : Je kuna yeyote anayejali ?- UNICEF

13 Agosti 2018

Je kuna mtu yeyote anayejali? Ukatili dhidi ya watoto unaendelea ! Ndivyo anavyohoji Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, Geert Cappelaere.

Hoja ya Bwana Cappelaere ambayo ametoa leo kupitia chapisho la rangi ya hudhurungi ikiwa na maandishi yanayotiririka damu, na michoro ya familia inazingatia idadi kubwa ya watoto waliouawa katika siku chache zilizopita.

Mathalani anasema katika saa 36 zilizopita, watoto 28 wamethibitishwa kuuawa huko Idleb na Magharibi mwa Aleppo Kaskazini mwa Syria amhapo watoto 7 wanatoka familia moja.

Halikadhalika wiki iliyopita shambulio la kwenye basi lililokuwa limebeba watoto wa shule limesababisha vifo vya watoto 21.

Je kuna mtu yeyote anayejali? Ukatili dhidi ya watoto unaendelea

Mkurugenzi huyo wa UNICEF kanda ya  Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika amesema kama hiyo haitoshi, vituo vitatu vya afya vinavyopata msaada kutoka shirika hilo navyo vimeshambuliwa ambapo viwili  kati ya hivyo vinavyosaidia wanawake na watoto haviwezi kutoa tena huduma,

“Vita dhidi ya watoto nchini Syria vinaweka watoto wapatao milioni moja huko Idlib pekee hatarini,” amehitimisha Bwana Cappalaere.

UNICEF
Mtoto akiwa ameketi kwenye dawati ndani ya moja ya darasa la shule iliyoshambulia huko Idleb nchini Syria mwaka 2016

Juliette Touma ambaye ni mkuu wa mawasiliano wa UNICEF kanda ya  Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini akihojiwa na Idhaa ya kiarabu ya Umoja wa Mataifa anafafanua kwa kina taarifa hiyo.

(Sauti ya Juliette Touma)

“Tunaposema vita dhidi ya watoto tuna maana kuwa  watoto wanashambuliwa, ina maana haki zao za msingi zinashambuliwa, wananyimwa haki zao za msingi. Hii iko maeneo mengi kwenye ukanda huu, iwe ni kupoteza makazi, kushindwa kupata huduma muhimu kama elimu, afya kwenye maeneo kama Libya, Yemen, Palestina Sudan. Kwenye ukanda wote kuna takribani watoto milioni 30 ambao wanahitaji misaada ya kibinadamu.”

Nchini Syria vita vya vilivyodumu kwa miaka minane sasa pamoja na huko Yemen mapigano yaliyoanza mwaka 2015 yamezidi kusigina haki za msingi za mtoto za kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa.

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter