Mkataba wa haki za mtoto ukitimiza miaka 30, haki za mtoto Yemen mashakani

Mtoto akitabasamu wakati anapokea chanjo za surua na Rubella wakati kampeni ya chanjo iliyowezeshwa na UNICEF kwenye jimbo la Aden nchini Yemen 2019
UNICEF/Mahmood Fadhel
Mtoto akitabasamu wakati anapokea chanjo za surua na Rubella wakati kampeni ya chanjo iliyowezeshwa na UNICEF kwenye jimbo la Aden nchini Yemen 2019

Mkataba wa haki za mtoto ukitimiza miaka 30, haki za mtoto Yemen mashakani

Haki za binadamu

Nchini Yemen, muhula mpya wa shule ukianza huku mzozo ukiendelea, watoto milioni 2 hawawezi kwenda shule, idadi ikijumuisha nusu milioni ambao ni watoro wa shule tangu mzozo uanze nchini humo mwaka 2015.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema idadi hiyo ikiwa hawako shuleni, mustakabali wa watoto wengine milioni 3.7 uko mashakani ukitegemea malipo ya mishahara ya walimu ambayo haijalipwa kwa zaidi ya miaka miwili.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen Beysolow Nyanti amenukuliwa katika taarifa ilyotolewa leo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Yemen akisema kuwa mapigano, ukosefu wa maendeleo na umaskini vimepora haki ya elimu na matumaini ya mamilioni ya watoto nchini humo.

Kama hiyo haitoshi amesema, ghasia, ukimbizi na mashambulizi dhidi ya shule vinazuia watoto kwenda shuleni huku mishahara ya walimu haijalipwa kwa miaka miwili sasa, akisema, “elimu bora kwa watoto Yemen iko mashakani.”

Kwa miaka minne sasa, mzozo unaoendelea nchini Yemen umesambaratisha mfumo wa elimu nchini Yemen ambao tayari ulikuwa umeporomoka huku shule moja kati ya tano haziwezi kutumika tena kutokana na mapigano yanayoendelea.

 “Miaka 30 iliyopita mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC,  uliridhiwa, na sasa haikubaliki kuwa elimu na haki nyingine za msingi za mtoto zinasalia ndoto nchini Yemen kwa sababu ya vitendo vya binadamu,” amesema Nyanti.

Amesisitiza kuwa watoto wanapokuwa hawako shuleni, wanakabiliwa na hatari lukuki ikiwemo utumikishwaji, ndoa za umri mdogo, ghasia na ukiukwaji wa haki zao nyingine za msingi.

Huku akisema kuwa UNICEF kwa ushirikiano na wadau wengine wanahaha kuhakiksha watoto Yemen wanapata haki yao ya elimu, mwakilishi huyo ametaka hatua za dharura zichukuliwe kuepusha watoto kukosa haki hiyo adhimu.

Hatua hizo ni pamoja na kukoma kushambulia shule na kulinda watoto na walimu, mamlaka za elimu Yemen zishirikiane kusaka mbinu za kulipa walimu mishahara yao na jamii ya kimataifa na wadau wa maendeleo wasaidie hatua za kuwapatia motisho walimu sambamba na kusaka suluhu ya kudumu ya mzozo nchini Yemen.

Mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC ulipitishwa miaka 30  iliyopita  ukitaja haki kuu nne za msingi ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kushirikishwa na kulindwa.