Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Adhabu ya kifo sio kigezo cha kumaliza ugaidi Misri

Adhabu ya kifo sio kigezo cha kumaliza ugaidi Misri

Pakua

Umoja wa Mataifa umeshtushwa na taarifa kuwa ndani ya wiki moja watu 20 wamenyongwa hadi kufa huko nchini Misri baada ya kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi nchini humo.

Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Liz Throssell amesema hayo hii leo mbele ya waandishi wa habari huko Geneva Uswisi.

Amesema Umoja wa Mataifa unaishauri serikali ya Misri kuangalia upya mwenendo wake wa kutoa adhabu ya vifo kwa watu wanaotuhumiwa na kisha kuhukumiwa kwa makosa ya mashambulizi ya kigaidi.

Mbali na changamoto za kiusalama zinazoikabili nchi hiyo hususan katika eneo la Sinai lakini uamuzi wa matumizi ya mahakama ya kijeshi kuendesha kesi na kisha kuhukumu kifo haitoi uwazi wa mwenendo wa kesi na kumnyima mtuhumiwa haki ya kujitetea hususan wale wanaipiga serikali au wakisiasa

Hivyo Bi. Throssell amesema Misri inapaswa kuzingatia kifungu namba 14 cha Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya haki za kiraia na kisiasa.

Photo Credit
Baraza la Haki za binadamu ambako wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa huwasilisha ripoti zao na kujadiliwa. (Picha:UN /Pierre Albouy)