Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkakati wa kimataifa wa bima wazinduliwa kukabili mabadiliko ya tabia nchi:Thiaw

Mkakati wa kimataifa wa bima wazinduliwa kukabili mabadiliko ya tabia nchi:Thiaw

Pakua

Mkakati wa kimataifa wenye lengo la kutoa bima kwa watu wasiojiweza na masikini zaidi ya milioni 400 ifikapo mwaka 2020 umezinduliwa leo mjini Bonn Ujerumani.

Mkakati huo “bima ya mnepo kwa ajili ya mabadiliko ya tabia nchi na hatari ya majanga umeziduliwa wakati wa mkutano unaoendelea wa mabadiliko ya tabia nchi COP23 , ukizileta pamoja nchi tajiri za G20 kushirikiana na nchi 20  zilizo katika hatari zaidi au V20.

V20 ni kundi la mataifa 49 yaliyo katika hatari yakiwemo ya visiswa vidogo kama Fiji . Ibrahim Thiaw naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa Mazingira UNEP anasema bima hiyo itakuwa nyota ya jaha kwa watu hao kwa sababu

(THIAW CUT 1)

“Tumeshuhudia matukio mbaya hususani mwaka huu yakiathiri kabisa uchumi, kusambaratisha visiwa mfano Jamhuri ya Dominica, pia tumeona Marekani, India na Pakistan , dunia leo iko katika taharuki na haitowezekana kwetu sisi kuangalia tu kinachotokea ni lazima tuchukue hatua tujipande ili matukio mengine yatakapotokea na yatakuwepo mengi tusishuhudie uharibifu mkubwa kama tunaouona sasa.”

Amesema tayari katika baadhi ya nchi watu wameshaanza kukata bima kwa kutambua kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi majanga mengi ikiwemo vimbunga, mafuriko na ukame yataendelea kutokea na kusababisha athari kubwa . Kuhusu bara la Afrika Thiaw amesema

(THIAW CUT 2)

“Afrika ni bara linaloendeshwa na sekta mama, sekta ya kilimo, uvuvi na kadhalika na athari hizi za majanga zinashusha uzalishaji na kila uzalishaji unapokwenda chini uchumi unakwenda chini , kwa hivyo itakuwa muhimu sana kwa serikali kwanza kuelewa na kwa jamii kuelimishwa vyema lakini wakati huohuo sekta binafsi kuja kuwekeza katika miundombinu ya kilimo ambayo inaweza kunepa mabadiliko ya tabia nchi.”

Photo Credit
Madhara ya mabadiliko ya tabianchi, hasa ukame wa muda mrefu katika Afrika inasababisha kuongezeka kwa njaa ya kimataifa. Picha: UM