Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfululizo wa mashambulizi Yemen unasikitisha-OHCHR

Mfululizo wa mashambulizi Yemen unasikitisha-OHCHR

Pakua

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeelezea wasiwasi wake kufuatia mfululizo wa mashambulizi nchini Yemen katika kipindi cha wiki moja iliyopita ambapo makumi ya raia wameuawa wakiwemo watoto.

Ofisi hiyo imetaka pande husika kwenye mzozo huo kuzingatia sheria ya kimataifa ambayo inalinda raia wakati wa mzozo na mashambulizi dhidi ya raia au mali zao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, Uswisi msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Rupert Colville amesema kumekuwa na mashambulizi kuanzia Novemba Mosi huku yakisababisha vifo na kuwaacha watu wengi majeruhi.

(Sauti ya Rupert)

“Tangu kurushwa kwa kombora Jumamosi, kumekuwa na mashambulizi tisa ya anga katika mji wa Sana’a unaoshikiliwa na wahouthi ikiwemo moja ambalo lilijeruhi raia watatu. Wakati walengwa wa mashambulizi sio wazi, tuna wasiwasi kwamba mashambulizi katika maeneo kuliko na watu wengi na mali ikiwemo miundombinu kuna hatari kubwa.”

Bwana Colville ameongeza kwamba wana wasiwasi kwamba msaada wa kibinadamu kwa ajili ya raia wasio na hatia huenda ukaathiriwa kufuatia hatua ya kufunga njia zote za kuwasili nchini humo ikiwemo kupitia barabara, anga na bandari.

Tayari Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema atateua kundi la wataalam kwa ajili ya kutathmini kwa kina ukiukaji wa haki za binadamu kimataifa na sheria ya kimataifa unaotekelezwa na pande husika kwenye mzozo.

Photo Credit
Familia waathirika wa mashambulizi nchini Yemen. Picha: OHCHR