Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano wahitajika kutatua matatizo ya usalama na wakimbizi:Sudan

Mshikamano wahitajika kutatua matatizo ya usalama na wakimbizi:Sudan

Pakua

Mshikamano wa kimataifa wahitajika ili kutatua changamoto za usalama, suala la wakimbizi na ugaidi. Hayo yamesemwa na waziri wa mambo ya nje wa Sudan Ibrahim Ahmed Abd al-Aziz akihutubia mjadala wa wazi wa baraza kuu hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Bwana Al-Aziz amesema Sudan bado inakabiliwa na changamoto kubwa hasa kwenye jimbo la Darfur ambako makundi ya waasi yamendelea kukabiliana na vikosi vya serikali na kusababisha madhara kwa raia.

Hata hivyo amesema Sudan hivi sasa imegeuza ukurasa kutoka machafuko na kuelekea amani , akiushukuru Mpango wa Umoja wa mataifa na Muungano wa Afrika UNAMID , Jumuiya ya nchi za Kiarabu, Muungano wa Afrika, na wadau wengine wa kimataifa walioisaidia nchi hiyo katika kipindi kigumu cha ghasia. Ametoa wito wa mshikamano zaidi kutoka nchi za Afrika katika kutatua matatizo ya Afrika.

Kuhusu suala la wakimbizi amesema nchi hiyo pamoja na kwamba ina wakimbizi wa ndani lakini imekuwa ikihifadhi wakimbizi wengi kutoka nchi jirani ikiwemo Sudan Kusini hali ambayo imeleta changamoto hasa katika suala la usaidizi wa kibinadamu na kutoa wito kwa jumuiya ya Kimataifa kuendelea kusaidia kutatua mzozo wa Sudan Kusini na kwingineko lakini pia kuongeza msaada kwa wakimbizi.

Ameguasia pia suala la usalama wa Kimataifa akisema Sudan inaungana na jumuiya ya kimataifa katika kupiga vita ugaidi katika mifumo yote , akiongeza kuwa hilo ni tishio la usalama wa kimataifa linalohitaji nguvu ya pamoja ya kimataifa.

Photo Credit
Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Ibrahim Ahmed Abd al-Aziz akihutubia kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa leo Jumamosi. Picha:Wen TV screen shot