Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano kwa Ethiopia sio tu wema bali ni haki na haja:Guterres

Mshikamano kwa Ethiopia sio tu wema bali ni haki na haja:Guterres

Pakua

Mshikamano kwa mahitaji yanayoikabili Ethiopi hivi sasa sio tu ni utu wema bali ni haki na haja ya kufanya hivyo. Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye kikao cha ngazi ya juu kuhusu hali ya kibinadamu nchi Ethiopia kilichofanyika Jumapili kwenye mkutano wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa.

Guterres amesema ni haki kutokana na ukarimu wa watu wa Ethiopia ambao kwa miaka mingi wamekuwa wenyeji wa kuhifadhi wimbi kubwa la wakimbizi Afrika ikifungua sio tu mipaka yake bali milango ya watu wake hata katika kipindi kigumu cha usalama, hasa ukizingatia wakati huu ambapo mipaka mingi inafungwa kutoruhusu wakimbizi.

Pia imetoa fursa kwa vijana wengi kutoka Eritrea, Somalia na Sudan Kusini ambao tayari wamepata diploma au wako katika vyuo vikuu vya serikali ya Ethiopia.

Hivyo ameongeza ni haki kwa Ethiopia ambayo sasa inakumbwa na zahma ya ukame ingawa ilijiandaa vyema tatizo limezidi uwezo wake kustahili kupatiwa msaada.

Amesema serikali, mashirika na wahisani wote wanafanya kazi ili kushughulikia mahitaji ya haraka ya kibinadamu lakini pia suluhu ya muda mrefu ya kuijengea uwezo Ethiopia kuweza kukabiliana na changamoto nyingi zinazoikumba nchi hiyo ya pembe ya Afrika hivi sasa.

Kwa upande mwingine Bwana Guterres amesema ni suala la haja kwa sababu uhusiano baina ya masuala ya kibinadamu na maendeleo kwa amani na usalama unazidi kukua kila mahali.

Na kuwekeza katika kuijengea uwezo jamii na katika mahitaji muhimu ya kibinadamu katika wakati wa uhitaji kama sasa ni kuchangia pia katika kuimarisha amani na usalama.

Ethiopia imekuwa muhimili katika pembe ya Afrika ukizingatia nchi nyingi zina zahma kubwa zaidi kama Somalia, Eritrea na Sudan Kusini, hivyo Guterres amesisitiza “hatuwezi kuruhusu athari za ukame kuchagiza madhila ya kutokuwepo usalama, machafuko na vita kwani vitakuwa na athari kubwa sana sio tu kwa ukanda huo bali kwa dunia kwa ujumla.”

Ametoa wito wa kushikamana sio tu kushughulikia mahitaji ya kibinadamu ya Ethiopia bali changamoto za maendeleo, amani na usalama kwa mtazamo wa yale yanayoighubika dunia hivi sasa.

Photo Credit
Jengo la Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia. Picha na AU