Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muhtasari wa habari: Walinda amani DRC, Wakimbizi Sudan, Homa ya ini

Helkopta za MONUSCO zikizunguka Ituri DRC (Kutoka Maktaba)
MONUSCO/Nazar Voloshyn
Helkopta za MONUSCO zikizunguka Ituri DRC (Kutoka Maktaba)

Muhtasari wa habari: Walinda amani DRC, Wakimbizi Sudan, Homa ya ini

Amani na Usalama

Baada ya huduma ya  ulinzi wa amani kwa zaidi ya miaka 20 huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC chini ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, walinda amani kutoka China, hii leo wameondoka katika kambi yao iliyoko nje kidogo ya mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, Bukavu ambako walishiriki kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miundombinu. 

Kuondoka kwao ni sehemu ya mpango wa MONUSCO kufunga virago DRC kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo ujumbe huo unatakiwa uwe umekamilisha majukumu yake mwezi Desemba mwaka huu.

Sudan

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Olga Sarrado Mur katika mkutano na waandishi wa habari leo mjini Geneva, Uswisi ameeleza kwamba vita nchini Sudan ikikaribia kutimiza mwaka mmoja kamili na ikiendelea kupamba moto, idadi ya Wasudan waliolazimika kukimbia sasa imepita watu milioni 8.5, huku milioni 1.8 kati yao wakiwa wamevuka mipaka ya nchi.

Homa ya ini

Na kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa leo, idadi ya watu wanaofariki dunia kutokana na virusi vya homa ya ini inaongezeka. Ugonjwa huo ni wa pili kwa kusababisha vifo vya watu milioni 1.3 kwa mwaka, sawa na ugonjwa wa kifua kikuu, ambao ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababisha vifo vingi zaidi kwa sasa. Hata hivyo WHO inasema lengo la kutokomeza  Homa ya ini ifikapo 2030 bado linapaswa kufikiwa.