Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres asema hofu imegeuzwa mtaji, ataja mambo 3 kutatua hali ya sasa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, (kulia) wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari leo Januari 18, 2019 kwenye makao makuu ya UN jijini New York
UN /Manuel Elias
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, (kulia) wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari leo Januari 18, 2019 kwenye makao makuu ya UN jijini New York

Guterres asema hofu imegeuzwa mtaji, ataja mambo 3 kutatua hali ya sasa

Masuala ya UM

Masuala ya hofu kuwa mtaji wa kisiasa, kauli za chuki, ukosefu wa usawa, ushirikiano wa kimataifa, mabadiliko ya tabianchi, maandamano huko Sudan na kwingineko duniani ni miongoni mwa mambo ambayo yamebeba mkutano kati ya Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na waandishi wa habari hii leo mjini New York, Marekani.

Mathalani kuhusu hofu, Bwana Guterres kwenye mkutano huo ambao ni wa kwanza kabisa kwa mwaka huu wa 2019, Guterres amesema inazidi kushamiri na ni kitu ambacho kimepewa thamani ya juu na husababisha watu kushinda kura.

“Na hivyo naamini changamoto kubwa ambayo serikali na taasisi zinakabiliwa nayo hivi sasa ni kuonyesha kuwa tunajali—kuhamasisha majawabu ambayo yanajibu hofu na wasiwasi wa jamii.”

Majibu kwa UN ni matatu

Amesema kwa Umoja wa Mataifa majawabu hayo ni matatu, mosi ni kuonyeshana kutekeleza harakati zake za kuhakikisha  hakuna mtu anaachwa nyuma kwenye maendeleo na msingi mkuu ni ajenda 2030 ya maendeleo endelevu.

Pili amesema ni kudhihirishia umma kuwa Umoja wa Mataifa unajali, na akatoa mfano wa hatua muhimu za mwaka jana kama vile mikataba ya wakimbizi na wahamiaji.

Hofu inazidi kushamiri, hofu inafanya watu washinde kura, hofu imepewa thamani ya juu- Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN

Adama Dieng kuandaa mkakati wa haraka kudhibiti kauli za chuki

Suala la tatu ni kushughulikia kauli za chuki ambazo amesema zinazidi kusambaa, watu wakisahau kile ambacho kauli za chuki kilisababisha miaka ya 1930.

“Tunahitaji kushirikisha kila jamii kwenye vita ya maadili inayokabili dunia yetu hivi sasa na hususan, kushughulikia ongezeko la kauli za chuki, chuki dhidi ya wageni na ukosefu wa stahmala. Kauli za chuki na uhalifu utokanao na kauli hizo ni tishio la moja kwa moja la haki za binadamu, maendeleo endelevu, amani na usalama.”

Amesema hatua bado hazitoshi kukabili kauli za chuki, hivyo amemwagiza Mshauri wake Maalum kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng, aandae jopo la Umoja wa Mataifa la kuchagiza hatua, kuainisha mkakati mpana zaidi na kuwasilisha hatua ya utekelezaji ya kimataifa ya kuchukua hatua haraka.

Ghasia nchini Sudan, "demokrasia au utulivu?"

Mwandishi mwingine akamuuliza Bwana Guterres maoni yake kuhusu hoja iliyopo hivi sasa huko Sudan ambako maandamano yanaendelea watu wakiulizwa iwapo wanachagua utulivu au demokrasia, ambapo amesema katu ni vigumu kuchagua kati ya vitu hivyo viwili. "Tunasihi kwa dhati serikali ya Sudan izingatie sana haki za binadamu na ijizuie katika njia zozote zile ambazo inataka kutumia kudhibiti maandamano haya kwa kuwa zinaweza kukandamiza haki hizo na bila shaka ni hatari kwa binadamu. Lakini tunaelewa pia kuwa licha ya machungu yanayokabili watu kuna hali ngumu ya uchumi na kama unavyojua Sudan iko katika hali mbaya kujinusuru na hili kwa kuwa kuna vikwazo lukuki. kwa hiyo naamini usaidizi wa kimataifa kwa Sudan ukihusishwa na ulinzi wa haki za binadamu na mazungumzo ya kisiasa ni itakuwa ni muhimu sana.

DRC na uchaguzi

Alipoulizwa kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako yadaiwa kuwa Muungano wa Afrika ambao umetaka kusitishwa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huko DRC,  Katibu Mkuu amesema anaamini kuwa si Muungano wa Afrika ndio umetoa uamuzi huo bali mkutano wa marais ulioitishwa na mwenyekiti wa AU na si uamuzi wa AU kama chombo lakini amesema "tunatumai hivi sasa kuwa mchakato wauchaguzi huko DR Congo utamamalizika  bila ghasia na kuheshimu utashi wa watu wa DRC na vyombo husika vya  uchaguzi. Na tunaamini kuwa hatua hizi na nyingine zozote zitachangia kwenye mwelekeo huu."