Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Homa ya ini huua watu 3,500 kila siku duniani kote, nchi zichukue hatua - WHO

Kuzuia maambukizi ya homa ya ini kwa njia ya chanjo za utotoni hupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizo sugu na visa vya saratani ya ini na cirrhosis katika utu uzima.
© WHO/Sri Lanka
Kuzuia maambukizi ya homa ya ini kwa njia ya chanjo za utotoni hupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizo sugu na visa vya saratani ya ini na cirrhosis katika utu uzima.

Homa ya ini huua watu 3,500 kila siku duniani kote, nchi zichukue hatua - WHO

Afya

Idadi ya watu wanaokufa kutokana na ugonjwa wa Homa ya Ini inaongezeka ambapo kwa sasa watu 3,500 wanakufa kila siku kutokana na ugonjwa huo, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO hii leo  huko Geneva, Uswisi.

Ripoti hiyo ya kimataifa kuhusu ugonjwa wa Homa ya Ini, inasema ugonjwa huo unaripotiwa kuwa ni wa pili duniani kwa kusababisha vifo vitokanavyo na maambukizi kwani kila mwaka watu milioni 1.3 wanakufa, ikiwa ni sawa na Kifua Kikuu, ugonjwa mwingine unaoongoza kwa maambukizi.

“Ripoti hii inatupatia taswira ya kuchukiza,” amesema Dkt. Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, akingeza kuwa, “licha ya maendeleo yaliyopatikana duniani kudhibiti maambukizi ya homa ya ini, idadi ya vifo inaongezeka kaw sababu ni watu wachache wenye ugonjwa huo ndio wanachunguzwa na kupatiwa matibabu.”

Hatua ya haraka kuleta mabadiliko

Ijapokuwa mbinu bora za kuchunguza na kutibu zinapatikana, na bei ya bidhaa zihusianazo na ugonjwa huo zinapungua, kasi ya kupima na kutibu imepungua, imesema WHO, kwenye ripoti hiyo iliyotolewa kwenye mkutano wa viongozi wa dunia kuhusu homa ya ini.

Hata hivyo, shirika hilo linasema kufikia lengo la WHO la kutokomeza homa ya ini ifikapo mwaka 2030 bado linaweza kufikiwa iwapo hatua za haraka zitachukuliwa.

WHO imejizatiti kusaidia nchi kutumia mbinu zote walizo nazo na zilizoko tena kwa bei nafuu ili kuokoa maisha na kubadili mwelekeo wa sasa wa ugonjwa huu,” imesema WHO.

© WHO/Isaac Rudakubana

Sehemu ya kusubiria matibabu katika Kituo cha Afya cha Musovu wilayani Bugesera, Rwanda. Chanjo ya hepatitis B katika dozi ya kuzaliwa ni asilimia 45 tu ulimwenguni, na chini ya asilimia 20 ya chanjo katika kanda ya Afrika ya WHO.
© WHO/Isaac Rudakubana
Sehemu ya kusubiria matibabu katika Kituo cha Afya cha Musovu wilayani Bugesera, Rwanda. Chanjo ya hepatitis B katika dozi ya kuzaliwa ni asilimia 45 tu ulimwenguni, na chini ya asilimia 20 ya chanjo katika kanda ya Afrika ya WHO.

Eneo la wagonjwa kusubiri katika kituo kimoja cha afya nchini Rwanda. Chanjo dhidi ya Homa ya ini aina ya B ni asilimia 45 tu duniani kote, ambapo katika nchi za Afrika ukanda wa WHO, utoaji wa chanjo hiyo ni chini ya asilimia 20.

Ongezeko la vifo

Zaidi ya watu 6,000 duniani kote wanaambukizwa homa ya ini kila uchao, imesema ripoti hiyo ya WHO.

Takrimu mpya kutoka nchi 187 inaonesha makadirio ya vifo kutokana na ugonjwa huo unaoambukiza kuongezeka kutoka milioni 1.1 mwaka 2019 hadi milioni 1.3 mwaka 2022. Katika vifo hivyo, asilimia 83 ni homa ya ini aina ya B, ilihali asilimia 17 ni homa ya ini aina ya C.

Makadirio mapya kutoka WHO yanadokeza kuwa watu milioni 254 waliishi na homa ya ini aina ya B na milioni 50 aina ya C mwaka 2022.

Nusu ya mzigo wa homa ya ini sugu aina ya B na C ni miongoni mwa watu wenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 54, ambapo asilimia 12 ni watoto. Wanaume ni asilimia 58 ya wagonjwa wote.

Kutokomeza janga la Homa ya Ini

Ripoti ya WHO inaainisha mlolongo w ahata za kuchukua ili kusongesha mwelekeo wa umma kuondokana na homa ya ini ifikapo mwaka 2030.

Hatua hizo ni pamoja na kupanua wigo wa kufikia  huduma za kupima na uchunguzi, kuimarisha huduma za msingi za king ana kuondokana na utungaji tu wa sera bali kutekeleza na hatimaye kuwa na tiba kamilifu.

Ingawa hivyo pengo la fedha linasalia kuwa changamoto, imesema WHO, ambapo kwa sasa mahitaji ni  mengi lakini fedha hni kidogo.

WHO inasema hiyo inasababishwa na mambo mbali mbali ikiwemo ukosefu wa hatua za gharama nafuu za kudhibiti ugonjwa huo, mbinu na changamoto lukuki za afya na hivyo homa ya ini kutopatiwa kipaumbele.

Ripoti inaainisha mikakati kwa nchi kushughulikia ukosefu wa uwiano na usawa katika kufikia mbinu za kinga na tiba kwa gharama nafuu.

Soma ripoti nzima hapa.

Fahamu kuhusu homa ya ini

Ugonjwa wa homa ya ini ugonjwa wa kuvimba kwa ini kunakosababishwa na maambukizi ya virusi na hatimaye kuleta matatizo ya kiafya, ambayo mengine yanaweza kusababisha vifo. Kuna aina tano za homa ya ini ambazo ni A, B, C, D na E. Ingawa zote zinasababisha ugonjwa wa ini , zinatofautiana mathalani njia ya maambukizi, ukali wake, maeneo ya kijiografia na mbinu za kinga.

Soma kwa kina hapa kuhusu homa ya ini.