Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa chakula shuleni wawawezesha wasichana kuepuka ndoa za utotoni

Wanafunzi wa kike nchini Sudan Kusini.
Education Cannot Wait
Wanafunzi wa kike nchini Sudan Kusini.

Msaada wa chakula shuleni wawawezesha wasichana kuepuka ndoa za utotoni

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP nchini Sudan Kusini kupitia programu yake ya chakula shuleni imefanikiwa kuwasaidi wasichana wengi kuepukana na ndoa za utotoni.

Sudan Kusini ni moja kati ya mataifa yenye viwango vya chini vya watu wanaojua kusoma na kuandika hususani kwa wasichana. Jamii katika taifa hilo la afrika ya mashariki huwaoza mabinti ikiwa ni njia moja wapo ya familia kujipatia mali na hivyo mtoto wa kike hujikuta akikosa haki yake ya msingi ya kupata elimu.

Huko Kapoeta Mashariki katika jimbo la Equatoria mashariki, shule moja ya msingi ambayo hatutaitaja jina imekuwa kimbilio la wasichana walio katka hatari ya kuolewa katika umri mdogo, mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo ni Grace mwenye umri wa miaka 16 anasema shule hiyo imekuwa nikama peponi.

“Nilipokuwa kijijini, wakati baba yangu alikuwa hai, maisha yalikuwa sawa na nilifurahia kila kitu maishani. Lakini mara baada ya baba yangu kufariki, hapo ndipo maisha yangu yakawa magumu, kaka yangu alitaka niolewe katika umri mdogo, na hapo ndipo maisha yakawa magumu”.

Grace anasema anachosikita ni kuwa watoto wa kike hawaheshimiki

“Kwa sababu mimi ni mtoto wa kike maisha ya kijijini sio mazuri, tunatazamwa kama chanzo cha utajiri, na sisi ndio tunalazimika kufanya kazi za mashambani, kitu chochote kinachohusiana na shule hakithaminiwi, na hawataki hata kujua ni nini. Wao wanaona kama kitu kisicho na maana, hawajui chochote kuhusu elimu, na hawako tayari kwa hilo”.

Hellen Locham ni mwalimu wa shule anayosoma Grace na anasema wamekuwa wakihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa shule kwa wasichana.

“Hawa wasichana wanaitwa "washindi" kwa sababu wasichana hawa wanalazimishwa kuolewa wakiwa na umri wa miaka 9, na wengine huposwa wangali wadogo, na walifanikiwa kukimbia vijijini, wakiteseka njiani na wamefanikiwa kuja shuleni”. Tumekuwa tukiwaambia watu ikiwa unapata msichana ambaye anapitia changamoto, msichana ambaye amelazimishwa kuolewa, wanaweza kupata elimu wanayotaka".

Mwalimu Hellen Locham anasema mbali na shule kupokea wasichana lakini wanalishukuru zaidi shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani kwa kuwawezesha kupata chakula shuleni. 

Chakula kuwa shuleni ni muhimu sana, ikiwa hakuna chakula na haujala kitu huwezi kuwa katika nafasi ya kuwa darasani, huwezi kufanya chochote, WFP imesaidia sana shule hii, wakati wa likizo hali inekuwa ngumu kwa wasichana hawa kuwa shuleni ikiwa hakuna chakula. Wengi wao wangaliweza kukimbia, wangaliweza kurudi makwao, wangesema bora niende kuteseka kuliko kufa hapa kwa njaa.

WFP inaendelea kusaidia wasichana walio hatarini zaidi kwa kuwaatia msaada wa chakula shuleni wakati wa likizo.