Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA yafanikisha wasichana bubu na viziwi kujikwamua

Mwanafunzi mwenye uoni hafifu akifanya mazoezi ya kutumia mashine ya nukta nundu kwenye shule ya watu wasioona ya Al-Noor  huko Mogadishu nchini Somalia.
UN Photo/Ilyas Ahmed)
Mwanafunzi mwenye uoni hafifu akifanya mazoezi ya kutumia mashine ya nukta nundu kwenye shule ya watu wasioona ya Al-Noor huko Mogadishu nchini Somalia.

MINUSCA yafanikisha wasichana bubu na viziwi kujikwamua

Utamaduni na Elimu

Msichana Theresa Kpana nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambaye ni bubu na kiziwi baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu kutokana na ukosefu wa miundombinu kwa watu kama yeye, sasa amechukua hatua ya kuunda kikundi cha wasichana 60  viziwi na bubu ili hatimaye wapate stadi za maisha na haki zao zilindwe kwa kuwa hivi sasa mustakabali wao uko mashakani.

Katika wilaya ya Combattant katika viunga vya mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Bangui ambako kuna jengo la makutano ya wanakikundi wa chama cha kitaifa cha viziwi na bubu. 

Changamoto za kundi hili katika jamii zinaongezeka zaidi kwa wasichana na ndipo Theresa Kpana mwenye umri wa miaka 24 akaamua kuunda kikundi cha wasichana bubu na viziwi na leo wamekutana wengine wakiwa katika mafunzo ya ushoni. 

Akizungumza kwa lugha ya alama huku mkalimani Herbet Amed akifafanua, Theresa anasema, “Tunafanya kazi mara kwa mara na viziwi kwa sababu kwanza tumegundua kuwa wameenguliwa katika jamii. Ndio maana tunahangaika kuhakikisha wanaondokana na kutengwa. Tunawasaidia kupata stadi za kazi mbalimbali.” 

Stadi hizo ni pamoja na ushoni ambapo wasichana hao viziwi na bubu wanaendelea na darasa. 

Takwimu za mwaka 2003 za taasisi ya kiuchumi na kijamii nchini CAR zilibaini kuwepo kwa viziwi na bubu 21,000 huku changamoto ikiwa hakuna hata shule moja ya msingi inayofundisha kwa lugha ya alama. 

Hii ikimaanisha kwamba si rahisi kwa mwanafunzi kiziwi kuingia sekondari na hata kupata stadi za kazi na hivyo kukwamisha ujumuishaji wao kwenye jamii. 

Theresa akizungumza kwa lugha ya alama huku akitafsiriwa na Herbet anasema, “Kama ningalikuwa na uwezo wa kuingia Chuo Kikuu, ningalisoma na kuwa daktari na hatimaye nisaidie mawasiliano ya matibabu kati ya madaktari na watu viziwi kama mimi. Mara nyingi hospitali tunakosa mawasiliano.”  

Kwa kuwa sasa wanakosa elimu ya shuleni, chama cha viziwi na bubu kinawapatia stadi kama vile za kilimo cha bustani, ufugaji wa kuku na ushoni wa nguo au vitambaa. 

Halikadhalika chama kinawawezesha kushiriki mafunzo ya afya ya uzazi yanayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi duniani, UNFPA,  mafunzo yanayoratibiwa na MINUSCA