Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlo shuleni huchochea akili za vijana, lakini walio hatarini zaidi bado wanaukosa: WFP

Watoto wakila chakula cha mchana kupitia programu inayohifadhiwa na WFP katika shule moja katika eneo la Omo Kusini nchini Ethiopia.
© WFP/Michael Tewelde
Watoto wakila chakula cha mchana kupitia programu inayohifadhiwa na WFP katika shule moja katika eneo la Omo Kusini nchini Ethiopia.

Mlo shuleni huchochea akili za vijana, lakini walio hatarini zaidi bado wanaukosa: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Takriban watoto milioni 420 kote ulimwenguni wanapokea mlo shuleni wakiwa ni  milioni 30 zaidi ya mwaka 2020  kwa mujibu wa ripoti mpya iliyochapishwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP.

Ripoti hiyo “Hali ya mlo shuleni duniani kote” inasema huku kukiwa na mgogoro wa sasa wa chakula duniani, na wakati familia nyingi zikijitahidi kuweka mlo mezani, serikali zinazidi kutambua thamani ya mipango hii yam lo shuleni.

Ni jadara muhimu la hifadhi ya jamii

Milo ya shuleni ni njia muhimu ya usalama kwa watoto na kaya zilizo katika mazingira magumu wakati ambapo takribani watu milioni 345 wanakabiliwa na viwango vya juu vya njaa, ikiwa ni pamoja na vijana na watoto milioni 153.

“Wakati dunia inapambana na mgogoro wa chakula duniani, ambao unahatarisha kuwaibia mamilioni ya watoto maisha yao ya baadaye, milo ya shuleni ina jukumu muhimu. Katika nchi nyingi ambazo tunafanya kazi, chakula anachopata mtoto shuleni kinaweza kuwa ndio chakula pekee anachopata siku hiyo,” amesema Carmen Burbano, mkuu wa programu za WFP za mlo shuleni.

Mlo shuleni ni muhimu hususan kwa watoto maskinia
WFP/Sierra Leone
Mlo shuleni ni muhimu hususan kwa watoto maskinia

Kujifunza kutoka kwenye janga la COVID-19

Ripoti hiyo ya WFP imesema nchi zimefanya kazi kubwa kurejesha programu za chakula cha mchana shuleni bila malipo kufuatia usumbufu uliosababishwa na janga la COVID-19 miaka mitatu iliyopita. “Hii imesaidia kuongezeka kwa wavulana na wasichana wanaopokea chakula shuleni, ambao wanawakilisha asilimia 41 ya watoto wote walio shuleni.”

Juhudi za kujikwamua kimataifa zilipokea msaada muhimu kutoka kwa “Muungano wa Chakula cha Shule” unaoongozwa na serikali, ambao ulioanzishwa mwaka 2020 ili kukabiliana na athari za janga hilo.

“Leo, hii serikali 75 ni wanachama wa muungano huo, ambao unalenga kuhakikisha kila mtoto anaweza kupata mlo wa kila siku, wenye lishe shuleni ifikapo 2030.” Imeongeza ripoti.

Uwekezaji mkubwa zaidi unahitajika

Hata hivyo, ripoti hiyo pia imeonyesha tofauti kati ya nchi tajiri, ambapo asilimia 60 ya watoto wa shule wanapata chakula, na mataifa yenye kipato cha chini, ambapo ni asilimia 18 pekee wanapata chakula.

“Hii ni asilimia nne chini ya viwango vya kabla ya janga la COVID-19, huku Afrika ikiorodhesha upungufu mkubwa zaidi.”

Ripoti hiyo pia imegundua kuwa baadhi ya nchi za kipato cha chini hazijaweza kujenga upya programu zao za kitaifa na zinahitaji msaada zaidi.

Katika nchi nane za Afrika, chini ya asilimia 10 ya watoto wa shule hupokea chakula cha bure au cha ruzuku shuleni.

Bi. Burbano amesema "Uwekezaji ni mdogo zaidi ambapo watoto wengi wanahitaji chakula cha shule zaidi. Tunahitaji kusaidia nchi za kipato cha chini katika kutafuta njia endelevu zaidi za kufadhili programu hizi. Hii itahitaji msaada wa muda mrefu kutoka kwa nchi wafadhili pamoja na ongezeko la uwekezaji wa ndani.”

Chakula cha shule kinachohifdhiwa na WFP kinagawiwa watoto nchini Ufilipino
© WFP/Rein Skullerud
Chakula cha shule kinachohifdhiwa na WFP kinagawiwa watoto nchini Ufilipino

Faida ni kubwa

Ripoti hiyo pia imeangazia faida mbali mbali za milo shuleni au chakula cha mchana bila malipo huwavutia wanafunzi wengi zaidi darasani, hasa wasichana, na huwasaidia kujifunza vyema wanapokuwa huko.

Wataalamu pia wamegundua kuwa mchanganyiko wa afya na elimu unawapa watoto katika nchi maskini njia bora ya kuondokana na umaskini na utapiamlo.

Zaidi ya hayo, utafiti umeonyesha kuwa programu zamlo shuleni zinaweza kuongeza viwango vya uandikishaji wa wanafunzi, pamoja na mahudhurio, kwa karibu asilimia 10.