Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani ya kudumu ni lazima Gaza asisitiza mkuu wa UN huku tishio la njaa likizidi kujongea

Wakati wa ziara ya mshikamano wa Ramadhani akizuru nchini Misri , Katibu Mkuu wa UN António Guterres
UN Photo/Mark Garten
Wakati wa ziara ya mshikamano wa Ramadhani akizuru nchini Misri , Katibu Mkuu wa UN António Guterres

Amani ya kudumu ni lazima Gaza asisitiza mkuu wa UN huku tishio la njaa likizidi kujongea

Amani na Usalama

Wakati njaa ikizidi kuidhoofisha Gaza, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo amerejea wito wake wa usitishaji mapigano wa kudumu kwa mzozounaoendelea Gaza na kuachiliwa huru kwa mateka wote waliosalia huku kukiwa na uharibifu usio na kifani na unaoendelea katika eneo hilo linalokaliwa la Palestina.

Akiwa mjini Amman, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman Safady, Bwana. Guterres amesema "Hitaji ni la dharura, huku akiahidi kuendelea kusukuma mchakato wa kuondolewa kwa vikwazo vyote vya misaada ya kuokoa maisha, kwa kuwezesha upatikanaji zaidi na vivuko zaidi vya kuingia Gaza. “

Ombi la mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa limekuja huku kukiwa na matukio ya kutisha yaliyoripotiwa na wahudumu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa misaada, hasa katika mikoa ya kaskazini, ambapo Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, limeripoti kwamba watoto 27 sasa wamekufa kutokana na matatizo yanayohusishwa na utapiamlo mkali au unyafuzi.

Guterres amesema "Lazima tukabiliane na ukweli. Hakutakuwa na suluhisho endelevu la kibinadamu kwa vita vinavyoendelea vya umwagaji damu kama hivi." 

Ameongeza kuwa "Napenda kurudia kwamba hakuna kinachohalalisha mashambulizi ya Oktoba 7 na utekaji nyara uliofanywa na Hamas na hakuna kinachohalalisha adhabu ya pamoja ya watu wa Palestina."

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakiwasilisha misaada huko Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNRWA
Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakiwasilisha misaada huko Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

UNRWA imezuiwa kupeleka msaada kaskazini Gaza

Ombi la Katibu Mkuu la kutaka kuwepo kwa amani ya kudumu na kusitishwa kwa mapigano kwa minajili ya kibinadamu ili kuwezesha utoaji wa chakula, mafuta na dawa kwa ufanisi limekuja huku shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, likithibitisha kuwa limezuiwa na mamlaka ya Israel kusafirisha msaada hadi kaskazini Gaza.

Wakati huo huo, shirika hilo la Umoja wa Mataifa ambalo ndilo mtoaji mkubwa wa misaada ya kimataifa katika eneo hilo liliripoti kwamba bidhaa za msingi katika majimbo ya kaskazini sasa "zimekuwa ghali mara 25 zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya vita, na mathalani kiroba cha kilo 25 cha unga kinagharimu zaidi ya dola 400.”

Licha ya maonyo kwamba njaa inakaribia Gaza, "hakujawa na mabadiliko makubwa katika kiasi chabidhaa zinazoingia Gaza au kuboreshwa kwa ufikiaji wa wenye uhitaji kaskazini,"limesisitiza shirika la UNRWA.”

Shirika hilo limebainisha kuwa katika siku 23 za kwanza za mwezi Machi, malori 157 tu ya misaada kwa siku yalivuka hadi Gaza, kwa wastani. 

“Hii ni chini ya uwezo wa usafirishaji wa msaada kuvuka mpaka na wa lengo la malori 500 kwa siku", kulingana na UNRWA.

Ucheleweshaji unaendelea kutokea katika kivuko cha Kerem Shalom kutoka Israel na huko Rafah kutoka Misri, limebainisha shirika hilo la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa mauaji ya polisi kadhaa wa Kipalestina katika mashambulizi ya anga ya Israel karibu na vivuko mapema mwezi Februari "yameathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa misaada.”

Mtto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya wakimbizi katika mji wa Rafah
© UNICEF/Eyad El Baba
Mtto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya wakimbizi katika mji wa Rafah

Msaada na matumaini kwa mamilioni ya watu

Hapo awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kwa mara nyingine umuhimu mkubwa wa UNRWA katika maisha ya mamilioni ya watu wakati hwa ziara yake hivi karibuni ambayo hufanya kila mwaka kwa ajili ya mshikamano wa kuadhimisha mwezi mtukufu wa Waislamu wa Ramadhani.

Guterres amesema "Lazima tujitahidi kudumisha huduma pekee muhimu ambazo hutolewa naUNRWA kwa sababu hiyo inaweka matumaini kwa mamilioni ya watu." 

Katibu Mkuu alisema hayo baada ya kukutana na wakaazi katika kambi ya wakimbizi ya Palestina ya Wihdat, makazi ya baadhi ya wakimbizi milioni 2.4 wa Kipalestina nchini Jordan ambayo ni idadi kubwa zaidi katika kanda.

Amesisitiza kwamba shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesalia kuwa "mstari wa matumaini na utu kwa wengi, ikileta tofauti halisi ambayo shule zake na vituo vya afya vinafanya kwa maisha ya wakimbizi wa Kipalestina wa rika zote.

Jukumu la ujenzi wa amani

Mbali na kutoa elimu kwa wasichana na wavulana zaidi ya 500,000, takriban watu milioni mbili wanapata huduma za afya na fursa zajira, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alieleza, akiongeza kuwa huku nusu milioni ya Wapalestina maskini zaidi pia wakinufaika na msaada huo. 

Mambo yote haya amesema yanachangia jukumu muhimu la UNWRA katika "kuendeleza mshikamano wa kijamii, kukuza utulivu na kujenga Amani. Fikiria ikiwa yote haya yangeondolewa hali itakuwa ya kikatili na isiyoeleweka, hasa tunapowaenzi wanawake na wanaume 171 wa UNRWA ambao wameuawa huko Gaza idadi ambayo ni kubwa zaidi ya vifo vya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika historia yetu."

Katika Ukanda wa Gaza, wakati huo huo, mashambulizi yameendelea bila kusitishwa mwishoni mwa juma, huku mashambulizi ya anga ya mabomu ya Israel yakiripotiwa kusini mwa Gaza, ikiwa ni pamoja na Rafah, ambako UNRWA inakadiria kuwa watu milioni 1.2 sasa wanaishi, "wengi katika makazi rasmi na yasiyo rasmi".

Mhudumu wa afya akimpatia matibabu mmoja wa watoto aliyejeruhiwa huko Ukanda wa Gaza
© WHO
Mhudumu wa afya akimpatia matibabu mmoja wa watoto aliyejeruhiwa huko Ukanda wa Gaza

Hofu ya wahudumu wa misaada wa zamani

Akielezea ziara yake kwenye kivuko cha mpaka cha Rafah mwishoni mwa juma, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema wahudumu wa misaada ya kibinadamu wa zamani aliokutana nao "hawajawahi kushuhudia kitu cha kutisha kama kile ambacho kimetokea huko Gaza. Kiwango na kasi ya vifo na uharibifu viko katika kiwango tofauti kabisa, na sasa njaa inawakabili Wapalestina huko Gaza." 

Amesisitiza kwamba kua ufahamu unaongezeka duniani kote kwamba yote haya lazima yasitishwe na suluhisho la Serikali mbili ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kumalizika kwa mzozo wa Israel na Palestina.”

Ameendelea kusema kuwa "Waisraeli lazima waone mahitaji yao halali ya usalama yakitekelezwa, na Wapalestina lazima waone matamanio yao halali ya kuwa na Taifa huru kabisa, linaloweza kuimarika na lenye mamlaka yanatimizwa, kulingana na maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na makubaliano ya awali." 

Dkt. Tedros ana wasiwasi kutokana na uvamizi mpya wa hospitali

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus pia alielezea wasiwasi wake leo huku kukiwa na ripoti kwamba vikosi vya Israel "vimezingira na kushambulia Hospitali ya Al-Amal katika mji wa kusini wa Khan Younis jana Jumapili.”

Amebainisha kuwa mfanyakazi wa Hilali Nyekundu wa Palestina na mtu mwingine mkimbizi wa ndani katika hospitali hiyo wameuawa.

"Shambulio lingine lililoripotiwa kwenye Hospitali ya Al-Amal huko Gaza, ni hali nyingine ambapo wagonjwa na wafanyikazi wa afya wako katika hatari kubwa," amesema Tedros kwenye ukurasa wa ke wa mtandao wa X, zamani Twitter akiongeza kuwa "Tunaomba ulinzi wao wa haraka na kurudia wito wetu wa kusitisha mapigano."

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa hapo awali lilisema kuwa timu ya WHO "haikupewa kibali kufika hospitali hiyo kutathmini mahitaji au kuhakikisha msaada kwa wagonjwa, ingawa iliweza kutoa maji na huduma ya kwanza kwa wafanyikazi tisa wa afya ambao walitembea kutoka Al-Amal hadi kusini mwa Gaza”.

Ripoti za vyombo vya habari jana Jumapili zilisema kuwa magari ya kijeshi ya Israel yalifika hospitali za Al-Amal na Nasser huko Khan Younis. 

Uvamizi kama huo hapo awali ulihalalishwa na Jeshi la Ulinzi la Israeli kuwa ni muhimu kuwatafuta wapiganaji wa Hamas.