Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nakaribisha juhudi za Misri katika kushighulikia mzozo baina ya Gaza na Israel: Wennesland

Wajumbe katika mkutano wa amani wa Cairo  ulioandaliwa na Misri
UN Photo/Eskinder Debebe
Wajumbe katika mkutano wa amani wa Cairo ulioandaliwa na Misri

Nakaribisha juhudi za Misri katika kushighulikia mzozo baina ya Gaza na Israel: Wennesland

Amani na Usalama

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati Tor Wennesland leo amekaribisha juhudi zinazofanywa na serikali ya Misri katika kushughulikia mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.

Katika tarifa yake iliyotolewa mjini Cairo Misri Tor amesema "Ninakaribisha juhudi za Misri kwa kuitisha mkutano wa leo wa Cairo wa amani kushughulikia uhasama unaoendelea huko Gaza na Israeli.”

Ameongeza kuwa pamoja na Katibu Mkuu, leo tumeendeleza mazungumzo ya kisiasa ya Umoja wa Mataifa na vyama husika katika kanda na kwingineko ili kukomesha umwagaji damu na kuzuia upotezaji zaidi wa maisha ya raia.

 Mratibu huo alisisitiza kuhusu wasiwasi ambao pia uko miongoni mwa wengi kuhusu hatari ya kutokea kwa mzozo katika eneo zima na kukaribisha wito wa wengi wa suluhisho la kisiasa kama njia ya kusonga mbele.

Asante kwa kuwezesha misaada kuingia Gaza

Pia Tor ameishukuru mamlaka ya Misri kwa kuwezesha hatua ya leo ya kuingiza misaada Gaza kupitia mpaka wa Rafah.

Amesema “Hii ni hatua muhimu ambayo haipaswi kuwa ya mwisho. Msaada unahitaji kutiririka kwa usalama na kila wakati kuendelea mbele.”

Amesisitiza kuwa “Gaza ni eneo la vita na mahitaji ni makubwa. Sisi sote tunaweza na tunapaswa kufanya mengi zaidi ili kuokoa maisha sasa.”

Amehitimisha ujumbe wake akisema “Nasisitiza ombi la dharura la Katibu Mkuu la kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote na kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa ajili yamasuala ya kibinadamu.”