Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UN aanza ziara ya mshikamano kipindi cha Ramadani huko Misri na Jordan

Watoto wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza wakiwa na taa kusherehekea mwezi tukufu wa Ramadhani.
© UNRWA
Watoto wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza wakiwa na taa kusherehekea mwezi tukufu wa Ramadhani.

Mkuu wa UN aanza ziara ya mshikamano kipindi cha Ramadani huko Misri na Jordan

Amani na Usalama

Kutokana na kuongezeka kwa mizozo na migogoro ya kibinadamu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameanza safari yake ya kila mwaka ya mshikamano kipindi cha Ramadhani, inayoanza wikendi hii mjini Cairo, Misri. Safari hiyo ambayo inasadifiana na mwezi mtukufu wa Ramadhani, inafanyika katika nyakati za misukosuko hasa kutokana na mzozo unaoendelea huko Gaza.

Katika utamaduni ambao ulianza alipohudumu kama Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR ili kuangazia jamii za Kiislamu zilizoko kwenye dhiki, Katibu Mkuu Guterres amewasili Cairo siku ya Jumamosi, ambako atasisitiza wito wake wa dharura wa kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu na kusitishwa kwa ghasia, hasa katika Ukanda waGaza na nchini Sudan. 

Ziara yake inasisitiza dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kushughulikia maswala ya kibinadamu katika maeneo yenye mizozo.

Wakati akiwa Misri, Katibu Mkuu atasafiri kuelekea kaskazini mwa Sinai, eneo ambalo limeathiriwa sana na migogoro. Huko, atatembelea hospitali ya El-Arish, akionesha mshikamano na wale walioathiriwa na ghasia. Zaidi ya hayo, atakutana na wafanyakazi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko Rafah upande wa Misri, kujadili mikakati ya kupunguza mateso ya wale waliokwama katikati ya mzozo.

Tweet URL

Safari ya kila mwaka ya mshikamano kipindi cha Ramadhani

Katika ishara ya mshikamano, Bw. Guterres atashiriki futari ya Ramadhani pamoja na wakimbizi kutoka Sudan, ambao wameikimbia nchi yao kutokana na uhasama unaoendelea.

Anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa amani na utulivu, haswa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kuzitaka pande zote kuzingatia usitishaji wa mapigano.

Aidha, Katibu Mkuu atashiriki katika majadiliano na viongozi wa Misri, kuendeleza juhudi za kidiplomasia kutatua changamoto za kikanda na kuhimiza ushirikiano katika kutatua migogoro.

Ziara za UNRWA nchini Jordan

Mara baada ya kumaliza mazungumzo yake mjini Cairo, Mkuu huyo wa UN ataelekea Amman, Jordan, kuendelea na safari yake ya mshikamano wakati wa Ramadhani. 

Akiwa nchini Jordan, atatembelea vituo vya shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, ambalo linatoa huduma muhimu kwa wakazi, akiangazia dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia jamii zilizo hatarini huku kukiwa na majanga.

Katika muda akaoakuwa mjini Amman, Katibu Mkuu atashiriki futari ya Ramadhani na wakimbizi wa Kipalestina na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, akisisitiza umuhimu wa huruma na umoja wakati wa shida.

Pia ameratibiwa kufanya mikutano na maafisa wa Jordan, akiimarisha juhudi za ushirikiano kushughulikia changamoto za kikanda na kukuza amani na utulivu.

Wakati dunia ikikabiliana na migogoro inayoendelea na dharura za kibinadamu, safari ya Katibu Mkuu Guterres ya mshikamano wa Ramadhani inatumika kama ukumbusho wa dhamira isiyoyumba ya Umoja wa Mataifa ya kushikilia kanuni za kibinadamu na kukuza amani katika mazingira magumu zaidi.