Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Hofu ya njaa yazidi kutawala baada ya watoto 10 kuripotiwa ‘kufa njaa’

Mtoto mwenye umri wa miaka minane akisubiri mgao wa chakula huko Rafah, kusini mwa Gaza. (Maktaba)
© UNICEF/Abed Zagout
Mtoto mwenye umri wa miaka minane akisubiri mgao wa chakula huko Rafah, kusini mwa Gaza. (Maktaba)

Gaza: Hofu ya njaa yazidi kutawala baada ya watoto 10 kuripotiwa ‘kufa njaa’

Msaada wa Kibinadamu

Tahadhari za mara kwa mara zilizokuwa zikitolewa na mashirika ya kibinadamu juu ya ukosefu wa uhakika wa chakula na hatihati ya kutokea kwa baa la njaa huko Gaza sasa limekuwa suala linaloangaziwa zaidi baada ya hii leo mamlaka ya eneo hilo kuripoti kwamba mtoto wa kumi almefariki kutokana na utapiamlo na upungufu wa maji mwilini.

“Rekodi rasmi jana au asubuhi ya leo zilisema kulikuwa na mtoto wa kumi aliyesajiliwa rasmi katika hospitali kama alikuwa na njaa hadi kufa," amesema msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO Christian Lindmeier ambaye ameeleza kuwa takwimu zisizo rasmi zinaweza kutarajiwa kwa bahati mbaya kuwa kubwa zaidi.

Taarifa hiyo imefuatia ripoti za vyombo vya habari jana usiku kuripoti kwamba watoto wanne walifariki katika hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza, pamoja na vijana wengine sita waliofariki Jumatano katika kituo kimoja na katika hospitali ya Al Shifa katika Jiji la Gaza.

"Janga" la njaa

Kuzidi kuzorota kwa ukosefu wa uhakika wa chakula katika eneo hilo - ambao ofisi inayohusika na uratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa OCHA ilisema umesababisha mtu mmoja kati ya wanne kukabiliwa na hali mbaya ya uhaba wa chakula - ulizusha hofu ya kimataifa siku ya Alhamisi, wakati zaidi ya Wapalestina 100 waliuawa na mamia kujeruhiwa wakijaribu kupata msaada kutoka kwenye msafara wa misaada uliosimama kwenye mzunguko kusini magharibi mwa jiji la Gaza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alilaani haraka tukio hilo na kutaka uchunguzi huru swala lililo ungwa mkono na maafisa wengine wakuu wa Umoja wa Mataifa akiwemo mkuu wa Umoja wa Mataifa wa misaada Martin Griffiths, huku kukiwa na ripoti za kuendelea mashambulizi makali ya Israel kutoka angani, nchi kavu na baharini kote eneo la Ukanda wa Gaza.

“Tuliona picha kutoka hospital ya Al Shifa ambapo waathirika wa mauaji walikuwa wamelala karibu karibu wakisubiri matibabu yoyote," Bw. Lindmeier wa WHO aliwaambia waandishi wa habari huko Geneva.

Kukatika kwa maji na umeme

“Mfumo wa Gaza - tumeusema mara nyingi kwamba uko kwenye magoti - ni zaidi ya magotini kwa sasa” Msemaji huyo wa WHO aliendelea kuwaeleza waandishi wa habari mjini Geneva  alipokuwa akielezea kwamba “njia zote za maisha za Gaza zimepunguzwa” - hasa maji na umeme - tangu mara baada ya mashambulio ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya jamii za Israeli tarehe 7 Oktoba.

Naye msemaji wa OCHA Jens Laerke wakati huo huo alisisitiza kuwa kabla ya mzozo “watu walikuwa na chakula, watu waliweza kuzalisha chakula chao.  Leo tofauti kupata chakula ndani ya Gaza yenyewe - iwe kutoka kwa kilimo au uvuvi - "ni vigumu sana", kuweka chakula mezani…kumekoma kabisa. Msingi wa watu kupata riziki kila siku unavunjwa.”

Msemaji huyo wa OCHA amesema tathmini za hivi karibuni za uhaba wa chakula zilizofanywa na mashirika ya kibinadamu - faharisi ya uainishaji ya IPC ambayo inatumiwa kama marejeleo na mashirika ya misaada - inaonesha kuwa wakazi wote wa Gaza (watu milioni 2.2) - wanakabiliwa na viwango vya "mgogoro" wa uhaba wa chakula. 

Kati ya idadi hiyo, karibu watu milioni 1.17 wanakabiliwa na viwango vya "dharura" vya uhaba wa chakula na hali mbaya, wengine 500,000 wanakabiliwa na "janga".

“Tuna hali mbaya inayotujia kwa kasi kubwa sana,” Bw. Laerke alisema, maoni yake yakirejea onyo la hivi karibuni la mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kwa Baraza la Usalama kwamba njaa katika eneo hilo 'inaweza kuepukika' isipokuwa kama msaada hautaongezwa kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa UNRWA, shirika la Umoja wa Mataifa linaloudumia wakimbizi wa Kipalestina, idadi ya misaada iliyofika Gaza mwezi Februari ilikuwa nusu tu ya jumla ya Januari – “na tunajua kwamba Januari haikutosha hata kidogo”, msemaji wa WHO alisema.

Ishara muhimu

Akirejelea wito wa mara kwa mara wa Umoja wa Mataifa wa kusitishwa kwa mapigano, Bw. Lindmeier alikumbusha kuwa vifo vilivyotokea wakati msafara wa misaada wa siku ya Alhamisi vilidhihirisha jinsi watu wa Gaza walivyokata tamaa kwa chakula, maji safi na mambo mengine muhimu, baada ya karibu miezi mitano ya vita.

“Hii ndiyo taswira halisi, hili ndilo janga la kweli hapa, kwamba chakula na vifaa vingine ni haba sana kwamba tunaona hali hizi zinajitokeza. Na chakula kimekatwa kwa makusudi,” alisisitiza, akibainisha kuwa wananchi wa Gaza hawakuwa na uwezo tena wa kujikimu.

“Mashamba yaliyokuwapo, yanahifadhi kilimo kidogo, yote yanahitaji maji, au usambazaji wa maji kulingana na umeme na vituo vya kusukuma maji,” alielezea. “Hii ndiyo taswira halisi; hii inasisitiza zaidi na zaidi kwamba tunahitaji usitishaji vita wa haraka sasa ikiwa sio sasa, basi lini?"