Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban wanawake 9,000 wameshauawa hadi sasa Gaza: UN Women

Wanawake wawili na mtoto wakiwa wameketi nje ya nyumba yao Gaza. Wazazi wengi hawawezi kukidhi mahitaji ya watoto wao ya kila siku kama chakula, maji, malazi ,afya na huduma zingine
WFP/Wissam Nassar
Wanawake wawili na mtoto wakiwa wameketi nje ya nyumba yao Gaza. Wazazi wengi hawawezi kukidhi mahitaji ya watoto wao ya kila siku kama chakula, maji, malazi ,afya na huduma zingine

Takriban wanawake 9,000 wameshauawa hadi sasa Gaza: UN Women

Amani na Usalama

Vita ya Gaza "pia ni vita dhidi ya wanawake", ambao wanaendelea kuteseka na athari zake mbaya, limesema shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake.

Shirika hilo UN Women, linakadiria kuwa wanawake 9,000 wameripotiwa kuuawa na vikosi vya Israel tangu vita ilipozuka karibu miezi mitano iliyopita. 

Hata hivyo, huenda idadi hiyo ikawa kubwa zaidi kwani wengi zaidi wanaripotiwa kufariki dunia kwa kufikiwa chini ya vifusi.

"Wakati vita hii haimuachi mtu yeyote, takwimu za UN Women zinaonyesha kwamba inaua na kujeruhi wanawake kwa njia ambayo haijawahi kushuhudiwa," shirika hilo lilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Ijumaa jioni.

Kwa kiwango cha sasa, wastani wa wanawake 63 wataendelea kuuawa ikiwa mapigano yataendelea.

Takriban akina mama 37 wanauawa kila siku, na kuacha familia zao zikiwa na ukiwa na watoto wao wakiwa na ulinzi duni.

Hofu ya njaa

Wiki hii, mashirika ya Umoja wa Mataifa yalionya Baraza la Usalama kuhusu njaa inayokuja huko Gaza, ambapo watu wote, takriban milioni 2.3, hivi karibuni watakabiliwa na kiwango kikubwa cha uhaba wa chakula ikiwa ni sehemu kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa.

Tathmini ya haraka iliyofanywa na UN Women kwa wanawake Wanawake 120, mwezi uliopita, ilifichua kuwa wengi, ambayo ni asilimia 84, walisema familia zao hula nusu au chini ya kile walichokuwa wakila kabla ya vita kuanza.

Ingawa akina mama na wanawake watu wazima wamepewa jukumu la kutafuta chakula, wao ndio wanaokula mwisho, kidogo na kwa uchache zaidi.

Mama mkimbizi wa ndani mwenye watoto wanne akiwa na watoto wake ndani ya hema kwenye chuo kikuu cha Al-Quds Gaza
© UNICEF/El Baba
Mama mkimbizi wa ndani mwenye watoto wanne akiwa na watoto wake ndani ya hema kwenye chuo kikuu cha Al-Quds Gaza

Akina mama hushinda njaa 

Wanawake wengi walionyesha kuwa angalau mtu mmoja katika familia alilazimika kuruka milo katika wiki iliyotangulia.

"Katika asilimia 95 ya kesi hizo, akina mama ndio wanakosa chakula, wakikosa angalau mlo mmoja ili kulisha watoto wao," imesema UN Women.

Takriban wanawake tisa kati ya 10 pia waliripoti kuwa ni vigumu kupata chakula kuliko wanaume. 

Wengine sasa wanakimbilia kutafuta chakula chini ya vifusi au kwenye mapipa ya takataka, au hatua zingine.

Usitishaji mapigano wa kibinadamu wahitajika sasa

Wakati huo huo, mashirika 10 kati ya 12 ya wanawake huko Gaza yameripoti kufanya kazi kwa kiasi fulani, kulingana na ripoti ya UN Women kuhusu masuala ya jinsia ya mzozo huo, iliyotolewa mwezi Januari.

"Endapo hakutakuwa na usitishaji mapigano wa haraka wa kibinadamu, basi watu wengi zaidi watakufa katika siku na wiki zijazo," limeonya shirika hilo.

Na kuongeza kuwa "Mauaji, mabomu na uharibifu wa miundombinu muhimu huko Gaza lazima vikome. Msaada wa kibinadamu lazima uingie na kuvuka Gaza mara moja.”