Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Kasi ya kufikisha misaada ya kiutu ni ndogo, yaonya WHO

Mhudumu wa afya akimpatia matibabu mmoja wa watoto aliyejeruhiwa huko Ukanda wa Gaza
© WHO
Mhudumu wa afya akimpatia matibabu mmoja wa watoto aliyejeruhiwa huko Ukanda wa Gaza

Gaza: Kasi ya kufikisha misaada ya kiutu ni ndogo, yaonya WHO

Amani na Usalama

Huko Ukanda wa Gaza, Mashariki ya Kati, kukiwa hakuna dalili za silaha kuwekwa chini, shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO hii leo limeendelea kusihi kupatikana kwa njia salama ya kufikisha misaada kwenye eneo hilo lililozingirwa na Israel ili kusaidia wananchi walionasa kwenye mzozo huo unaoendelea kwa siku 94 sasa. 

Mwakilishi wa WHO kwenye eneo linalokaliwa la Palestina, oPt, Dkt. Rik Peeperkorn akizungumza na waandishi wa  habari huko Geneva, Uswisi kwa njia ya video kutoka Yerusalem amesema “hata kama hakuna sitisho la mapigano, ungalitarajia njia za kupitisha misaada ya kiutu ziwe wazi kwa njia ambayo ni endelevu kuliko ilivyo hivi sasa.”

Amesema fursa ni finyu sana. Na muda unazidi kuyoyote kufikisha misaada hasa eneo la kaskazini mwa Gaza. 

Mtoto mwenye umri wa miaka minane akisubiri mgao wa chakula huko Rafah, kusini mwa Gaza
© UNICEF/Abed Zagout
Mtoto mwenye umri wa miaka minane akisubiri mgao wa chakula huko Rafah, kusini mwa Gaza

Kuomba chakula 

Misaada ya kiutu, hasa chakula inahitajika mno huko Gaza, hususan maeneo ya kaskazini, amethibitisha Sean Casey, Mratibu wa Timu ya dharura ya utabibu ya WHO, akizungumza na waandishi wa habari hii leo  huko Geneva, Uswisi kwa njia ya video kutokea Rafah, kusini mwa Gaza. 

“Hali ya upatikanaji wa chakula eneo la kaskazini ni mbaya, hakuna kabisa chakula. Kila mtu unayezungumza naye anaomba chakula. Anakusogelea na kukuuliza, ‘kiko wapi chakula?’ Watu wanatusaidia kufikisha vifaa ya matibabu. Lakini kila mara wanatuambia sisi tunapaswa turejee na chakula.” 

Akipazia wito huo na kuelezea wasiwasi awke kuhusu kushamiri kwa chuki kusini mwa Gaza, Dkt. Peeperkorn, amesema uamuzi wa kusafirisha watendaji na vifaa vya matibabu haraka na kwa usalama hauzingatiwi tena kwani kusitishwa kwa mzozo kunahitajika kwa operesheni zozote huko Gaza, ikiwemo eneo la kusini bila kuchelewa. 

Pamoja na kuhitajika kupeleka misaada zaidi Gaza, jambo lingine ambalo linahitajika kufanyika kwa dharura ni kusafirisha misaada ya kiutu na wafanyakazi ndani ya eneo lililozingirwa Gaza, “ili tuweze kufikia watu wengi zaidi kokote waliko,” amesema Dkt. Peeperkorn. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, watu 23,084 wameuawa katika eneo lililozingirwa la Gaza ambapo kati yao hao asilimia 70 ni wanawake na watoto. Takribani watu 59,000 wamejeruhiwa, idadi ambayo ni saw ana asilimia 2.7 ya idadi ya watu Gaza. 

UN iko tayari kabisa kutoa huduma 

WHO imesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa na wadau wake wamesalia tayari kusambaza misaada kwa wakazi wa Gaza, ambao wamevumilia kampeni ya mashambulizi ya mabomu inayofanywa na jeshi la Israeli, ikiwa ni kulipiza kisasi cha shambulio la kigaidi lililofanywa na wanamgambo wa kipalestina, Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba mwaka 2023, lililosababisha vifo vya watu 1,200 na wengine 240 walitekwa nyara. 

Kuendelea kwa uhasama pamoja na amri kutoka jeshi la Israel la kutaka watu wahame eneo la Gaza Kati na kusini huko Khan Younis, vinaendelea kukwamisha wagonjwa na magari ya wagonjwa kufika hospitali, amefafanua Dkt. Peeperkorn, akiongeza kuwa kwa sasa ni vigumu mno kwa WHO kufikisha vifaa vya matibabu na mafuta kwenye hospitali ambazo kwa sasa hazina vifaa hivyo.

Hospitali zenye hali mbaya zaidi ni zile zilizoko ukanda ambao watu wanatakiwa kuahma ambazo ni ile iitwayo European Gaza, Nasser na Al-Aqsa, hospitali zilizosalia kusini mwa Gaza kwa ajili ya watu milioni mbili, amesema Dkt. Peeperkorn.

Wafanyakazi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNOCHA, walitembelea hospitali ya Al-Aqsa huko Gaza na kuripoti kuona idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa wakiletwa kwa matibabu ya haraka, kufuatia mlipuko.
WHO Video
Wafanyakazi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNOCHA, walitembelea hospitali ya Al-Aqsa huko Gaza na kuripoti kuona idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa wakiletwa kwa matibabu ya haraka, kufuatia mlipuko.

Wahudumu wa afya waondoka ili kuokoa maisha yao 

“Suala la vifaa vya matibabu kushindwa kufikishwa maeneo husika na kuondolewa kwa madaktari wengi kutokana na hofu ya usalama vinachangia janga kuwa baya kwani kutababisha hospitali nyingi kutokuwa na wahudumu na hivyo zisifanye kazi kama ilivyo kaskazini mwa Gaza. Jamii ya kimataifa haipaswi kuacha hii iendelee,” ameonya Dkt. Peeperkorn.

Kiashiria kimoja cha “kupungua kwa fursa” ya kutoa huduma za kiutu na kuokoa maisha kwenye eneo hilo lililozingirwa ni kwamba kwa wiki mbili sasa WHO haijaweza kufika ukanda wa kaskazini mwa Gaza.

Jumla ya ziara 6 zilizopangwa na WHO kwenda eneo hilo tangu tarehe 26 Desemba zimefutwa. “Timu zetu ziko tayari kutoa huduma lakini bado hatujapokea vibali vinavyotakiwa kuendelea na safari kwa usalama,” amesema Mkuu huyo wa WHO kwenye eneo linalokaliwa la Palestina.