Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 2 ya vita Ukraine mamilioni wamesaidiwa na mamilioni bado wanahitaji msaada: IOM 

Timu tembezi za IOM zinafanya kazi za ukarabati katika mikoa kadhaa iliyoathiriwa pakubwa na makombora.
© IOM/Alisa Kyrpychova
Timu tembezi za IOM zinafanya kazi za ukarabati katika mikoa kadhaa iliyoathiriwa pakubwa na makombora.

Miaka 2 ya vita Ukraine mamilioni wamesaidiwa na mamilioni bado wanahitaji msaada: IOM 

Amani na Usalama

Miaka miwili tangu kuongezeka nchini Ukraine, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM limesaidia watu milioni 6.5 nchini humo na katika nchi 11 jirani, kwa kutoa misaada muhimu na kuokoa maisha kwa wale wanaohitaji zaidi msaada huo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa IOM Amy Pope "Uharibifu umeenea kila kona ya Ukraine, maelfu ya watu wamepoteza maisha na mateso yanaendelea. Pamoja na hayo yote, IOM imekuwa na uwepo wa mara kwa mara ndani ya Ukraine na katika nchi jirani, ikisaidia idadi kubwa ya watu wanaokimbia kuokoa maisha yao. Mahitaji ni makubwa, hata hivyo, n ani mengi zaidi ya uwezo wa kutimiza mahitaji hayo”.

Ameongeza kuwa zaidi ya watu milioni 14.6 sawa na asilimia 40 ya idadi ya watu wote wa Ukraine bado wanahitaji aina fulani ya msaada katika mwaka huu wa 2024, wakati wakimbizi milioni 2.2 wanahitaji msaada katika nchi Jirani walikokimbilia.

“Wakati miaka miwili itatimia keshokutwa tangu uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine, zaidi ya watu milioni 14 karibu theluthi moja ya wakazi wa Ukraine wamekimbia makazi yao. Familia zimetenganishwa, watoto wameachwa bila makao, na jamii zimeharibiwa.”Limesema shirika hilo la uhamiaji.

Na kuongeza kuwa watu wengine milioni 3.7 wamesalia kuwa wakimbizi ndani nchini Ukraine, wakati karibu wengine milioni 6.5 ni wakimbizi duniani kote na watu wengine zaidi ya milioni 4.5 wamerejea nyumbani hadi sasa kutoka nje ya nchi au kutawanywa ndani ya nchi.

Johannes Fromholt wa IOM akisaidia kupakua bidhaa za msaada huko Kurakhove katikati mwa Ukrainia.
© Johannes Fromholt
Johannes Fromholt wa IOM akisaidia kupakua bidhaa za msaada huko Kurakhove katikati mwa Ukrainia.

Tunashirikiana na serikali

Kwa mujibu wa IOM imekuwa ikifanyakazi na serikali, Umoja wa Mataifa na wadau wa mashirika ya kiraia ndani ya Ukraine na katika nchi jirani, nah atua za IOM zinatoa kipaumbele katika ulinzi wa watu walio hatarini zaidi. 

IOM inaunga mkono juhudi za uokoaji nchini Ukraine kwa kujenga upya mifumo ya makazi, maji, mifumo ya kupasha nyumba joto, na kutoa huduma za afya.

Msaada wa wafadhili kwa hatua hizo umekuwa mkubwa na IOM inatoa shukrani kwa mchango huo muhimu. 

Katika miaka miwili ya kwanza ya hatua za msaada dola milioni 957 zilikusanywa kati ya lengo la ufadhili lililokusudiwa la dola bilioni 1.5. 

Vita inapoingia katika awamu ya muda mrefu, hata hivyo, IOM imeonya kuwa  mahitaji yanaendelea kuongezeka na kupita rasilimali zilizopo.

Chondechonde wafadhili ongezeni msaada

Mkurugenzi mkuu Pope amesema "Tunategemea kuongezeka kwa msaada kutoka kwa wafadhili na washirika wa ndani ili kukabiliana na changamoto zilizopo katika kutoa maisha bora kwa Waukraine". 

Ameongeza kuwa IOM inaipongeza Serikali ya Ukraine na watu wa Ukraine kwa nguvu na ujasiri wao, pamoja na majirani wa Ukraine ambao wanawapokea wale wanaosaka usalama. 

Amesisitiza kuwa “Tunaendelea kujitolea kikamilifu kupunguza mateso ya watu wa Ukraine na na katika jitoihada za kujikwamua.”

Ameaihi kuwa IOM itaendelea na jukumu lake kama mshirika anayeaminika wa Muungano wa Ulaya, Serikali za Ukraine na nchi zinazohifadhi wakimbizi ili kusaidia watu walioathiriwa na vita hii inayoendelea.