Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita nchini Ukraine itaathiri vizazi na vizazi: UN Ripoti

Mama na watoto wake wawili wakijinkinga kutokana na mashambulizi ya mabomu katika kituo cha metro cha Kyiv mnamo Januari 2024.
© UNICEF/Aleksey Filippov
Mama na watoto wake wawili wakijinkinga kutokana na mashambulizi ya mabomu katika kituo cha metro cha Kyiv mnamo Januari 2024.

Vita nchini Ukraine itaathiri vizazi na vizazi: UN Ripoti

Haki za binadamu

Uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine, ukiingia mwaka wake wa tatu wiki hii, umesababisha "gharama ya kutisha ya binadamu na mateso makubwa kwa mamilioni ya raia ambayo yatahisiwa na vizazi na vizazi",amesema leo Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa  mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk.

Katika taarifa yake wakati akizindua ripoti mpya kuhusu Ukraine mjini Geneva Uswisi Türk amesema "Shambulio kamili la silaha la Urusi dhidi ya Ukraine, ambalo linakaribia kuingia mwaka wake wa tatu bila kuwa na dalili ya kukoma, linaendelea kusababisha ukiukwaji mkubwa na ulioenea wa haki za binadamu, na kuharibu maisha na uwezo wa watu kuishi.”

Mwezi huu unaadhimisha sio tu miaka miwili tangu kuanza kwa shambulio la Moscow, lakini pia miaka 10 tangu Urusi ichukue kinyume cha sheria Jamhuri ya Crimea ya Ukraine na mji wa Sevastopol.

Mamilioni wamekimbia makazi yao, maelfu wamekufa

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kufuatilia Haki za Kibinadamu nchini Ukraine umethibitisha majeruhi 30,457 ambao ni raia tangu tarehe 24 Februari 2022, wakiwemo  watu 10,582 waliouawa na 19,875 kujeruhiwa, huku idadi halisi ikiwezekana kuwa kubwa zaidi.

Mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao, maelfu wengine wamepoteza makazi yao, na mamia ya taasisi za huduma za matibabu na elimu zimeharibiwa vibaya au kusambaratishwa kabisa na kuathiri sana haki za watu za afya na kupata elimu.

"Athari za muda mrefu za vita hivi nchini Ukraine zitaonekana kwa vizazi na vizazi” amesema Bwana Türk alisema.

Ukiukwaji mkubwa wa haki

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR imeorodhesha mateso mengi, unyanyasaji na uwekaji kizuizini kiholela wa raia unaofanywa na vikosi vya jeshi la Urusi.

Utekelezaji wa mauaji, watu kutoweshwa na ukandamizaji wa haki ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika pia umeorodheshwa katika eneo linalokaliwa.

Kwa kuongezea, mahojiano  yaliyofanywa na ujumbe wa ufuatiliaji na wafungwa 550 wa zamani wa vita na wafungwa wa kiraia yameonyesha kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu na unaotekelezwa vikosi vya jeshi la Urusi, pamoja na mauaji ya kiholela na utesaji uliosambaa.

Tangu tarehe 24 Februari 2022, hali mbaya ya haki za binadamu katika eneo la Crimea linalokaliwa imezidi kuwa mbaya, huku kukiwa na msako mkali dhidi ya wale wanaokosoa uvamizi huo. 

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa itatoa ripoti kuhusu uvamizi wa Urusi uliodumu kwa muongo mmoja wiki ijayo.

"Shambulio linaloendelea la Urusi haliepushi majeshi ya Ukraine katika kutimiza majukumu yao ya kuheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu," amesema mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Vita nchini Ukraine vimesababisha uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu ya umma.
© EU/Oleksandr Rakushnyak
Vita nchini Ukraine vimesababisha uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu ya umma.

Amani inahitajika haraka

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Ofisi imeirodhesha pia idadi ya ukiukwaji uliofanywa na vikosi vya jeshi vya ulinzi na usalama vya Ukraine, pamoja na sehemu ya wigo wa ule ukiukwaji unaofanywa na vikosi vya Urusi, almesema, akibainisha kuwa Ofisi yake inaendelea kushirikiana na mamlaka ya Ukraine kushughulikia masuala haya.

Akirejelea wito wake kwa Urusi wa kusitisha mashambulizi yake yanayoendelea ya kijeshi dhidi ya Ukraine mara moja, amesisitiza udharura wa kupatikana kwa amani na haki na akatoa wito tena kwa Moscow kuruhusu OHCHR kupata fursa ya kufika na kutekeleza kikamilifu wajibu wake.

Komesha ukwepaji wa sheria ni pamoja na kifo cha Navalny

Mtaalamu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Urusi leo Alhamisi ametoa wito wa uwajibikaji na mshikamano na wahanga wote wa vita, wakiwemo wanaharakati  wa haki za binadamu wa Urusi.

Vita hivyo vimeathiri mamilioni ya watu wa Ukraine na kuzidisha ukandamizaji wa haki za kiraia na kisiasa ndani ya Urusi yenyewe na "kuanzisha vita dhidi ya Warusi nyumbani", amesema Mariana Katzarova katika taarifa yake ya.

Kufuatia habari za kifo cha kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny kilichotokea gerezani wiki iliyopita, yeye na wawakilishi wengine Maalum wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa Moscow kufanya uchunguzi huru na kuachiliwa mara moja kwa wafungwa wote wa kisiasa nchini Urusi.

Tangu Ijumaa iliyopita, mamlaka ya Urusi imewaweka kizuizini kwa jeuri na kiholela mamia ya raia walioandamana kwa Amani kuweka maua kwa heshima ya Navalny katika miji zaidi ya 39 kote Urusi, ameongeza Maria.

Amesema "Ninatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusimama katika mshikamano na wahanga wote wa vita dhidi ya Ukraine, wakiwemo watetezi shupavu wa haki za binadamu wa Urusi, waandishi wa habari na wanaharakati wanaoendelea kupinga vita kwa ujasiri licha ya kukabiliwa na vitisho, mateso, kifungo cha muda mrefu na hata kifo”.

Wawakilishi Maalum na wataalam wengine huru wa haki ni sehemu ya kile kinachojulikana kama Taratibu Maalum za Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa . 

Wao si wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, ni wawakilishi huru kutoka kwa serikali au shirika lolote na hawapati mshahara kwa kazi yao.