Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa Sudan ni tishio kwa ukanda mzima huku njaa na utapiamlo vikiongezeka: WFP

Familia zilizotawanywa na vita Sudan zikiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Aj Jazirah, Sudan.
© UNOCHA/Alimbek Tashtankulov
Familia zilizotawanywa na vita Sudan zikiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Aj Jazirah, Sudan.

Mgogoro wa Sudan ni tishio kwa ukanda mzima huku njaa na utapiamlo vikiongezeka: WFP

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP leo limeonya kwamba mgogoro wa Sudan unaleta tishio kubwa katika ukanda mzima wakati watu milioni 25 wakihaha kwa njaa, utapiamlo mkali na maelfu ya familia zikifurushwa makwao na wengine kulazimika kuvuka mpaka kwenda kusaka usalama nchi za jirani. 

Kwa mujibu wa Michael Dunford mkurugenzi wa WFP wa Kanda ya Afrika Mashariki akizungumza kutokea Kwenye mji wa mpakani wa Renk ambako watu laki tano wanaokimbia vita wamewasili amesema “Athari za vita ya Sudan imesambaa sio tu Sudan bali pia nchini Sudan Kusini na Chad na kuzusha mgogoro mkubwa zaidi wa watu kutawanywa duniani. Ikiwa ni takriban mwaka mmoja tangu kuzuka vita Sudan hatuoni dalili yoyote ya kupungua kwa idadi ya familia zinazofungasha virago na kukimbia nchi jirani.”

Pia amesema watoto na wanawake ndio waathirika wakubwa na wale wanaowasili Sudan Kusini au Chad wanawsili bila chcochote na wakiwa na njaa.

WFP inasema njaa na utapiamlo vimeongezeka nchini Sudan tangu mzozo huo uanze. Kuna watu milioni 18 wenye uhaba wa chakula na karibu watoto milioni 3.8 walio na chini ya umri wa miaka 5 wana utapiamlo. 

Na wengi wamekwama katika maeneo yenye mapigano makali ambapo WFP na mashirika mengine ya misaada yanajitahidi kuwa na ufikiaji thabiti ili kuwapa msaada unaohitajika. 

Wanawake na wasichana wakichota maji kwa ajili ya familia zao katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan.
© UNICEF/Adriana Zehbrauskas
Wanawake na wasichana wakichota maji kwa ajili ya familia zao katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan.

Wengi wanaendelea kufungasha virago

Wale ambao wanaweza kutoroka wanakimbilia maeneo kama Sudan Kusini au Chad, na kuongeza hali mbaya ya kibinadamu katika nchi hizo mbili ambazo tayari zinakabiliwa na changamoto.

Kwa wale wanaowasili sasa Sudan Kusini mathalani wanajiunga na familia ambazo tayari zinakabiliwa na mgao mdogo  wa chakula na njaa kali.

Pia utapiamlo unaongezeka kwa kasi miongoni mwa watoto wanaoteseka katika kambi za muda za wakimbizi. 

Takwimu za WFP zinaonyesha kuwa takriban asilimia 4 ya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 wanaovuka mpaka na kuingia Sudan Kusini wana utapiamlo wanapowasili. 

Lakini, takwimu hizi zinaongezeka hadi asilimia 25 miongoni mwa watoto katika kituo cha mpito cha Renk karibu na mpaka wa Sudan-Sudan Kusini, na shirika hilo linaonya kwamba jinsi watu wanavyokaa katika kambi za muda, ndivyo wanavyokuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na utapiamlo.

Wanawake na watoto waliokimbia makazi yao katika eneo la Wakimbizi wa Ndani huko Darfur Magharibi kutokana na mapigano nchini Sudan.
© UNOCHA/Mohamed Khalil

Hatua zisipochukuliwa sasa itakuwa zahma kubwa

Dunford ameonya kwamba “endapo mzozo huo wa Sudan hautopatiwa ufumbuzi, fursa kutolewa kwa mashirika ya msaada wa kibinadamu na kupatikana kwa fedha za ufadhili basi hali itakuwa janga kubwa la kibinadamu.”

 Ameongeza kuwa “Tunahitaji kuweza kuzisaidia familia ndani ya Sudan ili kuzuia mgogoro wa kihistoria wa watu kutawanywa kuwa janga lisilowezakudhibitika duniani hasa tunapojengea msimu wa muambo.” 

Nchini Chad, WFP inasema zaidi ya Wasudan 553,000, wengi wao kutoka Darfur, wamekimbia na kuingia nchini humo tangu mzozo huo kuanza. 

Takriban asilimia 40 ya watoto wakimbizi walioletwa kwenye kliniki ya dharura katika kambi ya mapokezi walionekana kuwa na utapiamlo mkali. 

Mama kutoka Sudan na watoto wake wanapata hifadhi katika mji wa Chad katika mpaka wa Darfur nchini Sudan.
© UNICEF/Annadjib Ramadane Maha
Mama kutoka Sudan na watoto wake wanapata hifadhi katika mji wa Chad katika mpaka wa Darfur nchini Sudan.

Utapiamlo umefurutu ada

Kiwango cha utapiamlo katika kambi nyingi za wakimbizi wa Sudan nchini Chad ikiwa ni pamoja na kambi za awali ni juu ya kiwango cha dharura cha shirika la afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO cha asilimia 15. 

WFP imelazimika kutoa kipaumbele kwa rasilimali chache kwa wanaowasili, ambao wengi wao wanavuka mpaka bila chochote. 

Hii ina maana kwamba wakimbizi waliokuwepo hapo awali hawapati tena usaidizi, lakini haimaanishi wako katika hali nzuri zaidi kuliko wale wanaowasili leo.

Janga kubwa la njaa linakaribia huku mahitaji ya chakula na lishe kote Sudan, Sudan Kusini na Chad yakiongezeka. 

Msaada wa kibinadamu ni muhimu na bado WFP inakabiliwa na pengo la karibu dola milioni 300 kwa muda wa miezi sita ijayo.