UNHCR yaomba msaada kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi nchini Sudan

14 Januari 2020

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR  lina mpango wa kuongeza msaada kwa Sudan kwa kutoa  ombi la dola milioni 477 kusaidia wakimbizi 900,000 nchini humo pamoja na karibu watu robo milioni wanaowapa hifadhi katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Mpango huo wa wakimbizi uliozinduliwa mapema leo mjini Khartoum, unahusu huduma za kibinadamu zinazofanywa na UNHCR na zaidi ya washirika 30. Sudan ina historia ya kuwahifadhi wakimbizi na wale wanaotafuta hifadhi lakini huwa inakumbwa na changamoto za wakimbizi wa ndania, wakati inakbiliwa na mzozo wa kiuchumi. Wito huo unakuja wakati nchi hiyo inapitia mabadiliko ya kisiasa, huku ikiwa inahitaji usaidizi wa kupata amani.

Kundi kubwa zaidi la wakimbizi waliopo Sudan ni kutoka Sudan Kusini ambapo wakimbizi 840,000 wanatafuta hifadhi nchini humo tangu mwaka 2013. Misaada pia inahitajika kwa wakimbizi kutoka nchi tisa ambao wametafuta hifadhi wakikimbia ghasia na mateso.

Katika kipindi hiki Sudan pia inaendelea kuwapokea wakimbizi wapya. Huko Darfur kuingia kwa wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya kati maeneo ya Kusini na kati kati mwa Sudan imechangia idadi kuongezeka kutoka wakimbizi 5,000 hadi 17,000 katika kipindi cha miezi mitatu tangu Septemba 2019. Babar Baloch ni msemaji wa UNHCR Geneva Uswis

(SAUTI YA BABAR BALOCH)

Licha ya wakimbizi kunufaika na misaada kutoka kwa jamii zinazowahifadhi, mzozo wa kiuchumi unaoshuhudiwa sasa umechangia hali kuwa mbaya kutokana na uhaba ya mahitaji.

Miaka kadhaa ya mizozo pia imechangia kuhama zaidi ya watu 600,00 raia wa Sudan kama wakimbizi kwenda nchi majirani ikiwemo wakimbizi 300,000 kutoka Darfur, mashariki mwa Chad.

Tangu makubaliano yatiwe sahihi kati ya serikali ya Sudan, Chad na UNHCR  mwezi Mei mwaka 2017, karibu wakimbizi 4000 kutoka Sudan wameamua kurudi nyumbani, zaidi wakitarajiwa kurudi mwaka huu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter