Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatuna jinsi bali kukatiza msaada Chad Aprili tukikosa fedha: WFP

Chakula kinagawiwa kwa wakimbizi wa Sudan huko Koufron, Chad.
© WFP/Jacques David
Chakula kinagawiwa kwa wakimbizi wa Sudan huko Koufron, Chad.

Hatuna jinsi bali kukatiza msaada Chad Aprili tukikosa fedha: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP hii leo linaonya kuwa litalazimika kusitisha misaada ya kuokoa maisha nchini Chad ifikapo mwezi ujao wa Aprili iwapo litakosa ufadhili wa haraka kwa ajili ya kusaidia wakimbizi.

Onyo hilo kali linakuja wakati maelfu ya wakimbizi wa Sudan wakiendelea kumiminika kuvuka mpaka kutoka Darfur, na wakati msimu wa mvua ukikaribia kuanza na hivyo kutishia kukatika kwa mawasiliano  kwa ajili ya utoaji wa misaada ya kibinadamu kwenye kambi za mashariki mwa nchi ambako mamilioni ya wakimbizi i kutoka Sudan wanasaka hifadhi eneo hilo. 

Katika tarifa hiyo ilityotolewa mjini N’Djamena WFP inasema watu milioni 1.2 wataathirika msaada huo ukisitishwa wengi wakiwa ni wakimbizi wa Sudan na watu walioathirika na mzozo unaoendelea wakiwemo wakimbizi wapya wa Sudan.

Na pia njia pekee ya kuingiza msaada Darfur inayoaminika Magharibi mwa Sudan itaathirika, Njia hiyo imesisaidia WFP kutoa msaada kwa watu milioni moja tangu mwezi Agosti mwaka jana kwenye jimbo la Darfur na shirika hilo linahaha kuhakikisha linafikisha msaada kwa watu milioni moja kwa mwezi.

Tishio la mvua za masika

Hivi sasa WFP inahaha kuhakikisha inakusanya, kusafirisha na kuweka akiba ya kutosha katika eneo la Mashariki mwa Chad ili kusambaza msaada kwa wakimbizi na kuendesha operesheni za mpakani mwa Darfur wakati wa msimu wa mvua za masika ambao utasabbaisha barabara kughubikwa na tope na malori mengi kukwama njiani na bila fedha za ufadhili hii itakuwa vigumu kutekelezwa.

Pierre Honnorat, mkurugenzi na mwakilishi wa WFP nchini Chad  amesema "Tunakimbizana na wakati. Diridha lililo wazi linakaribia kufungwa  kwa kasi na ufadhili wetu unakauka katika wakati huu muhimu. Tayari tumekatisha shughuli zetu kwa njia ambazo hazingewezekana miaka michache iliyopita, na kuwaacha watu wasio na chakula wakikaribia janga la njaa," 

WFP iko katika hatihati ya janga kubwa la ufadhili nchini Chad na tayari imepunguza kila mahali operesheni zake. 

Tangu mzozo nchini Sudan ulipozuka mwaka jana, ufadhili usio na uhakika umeifanya WFP kuzingatia mahitaji ya haraka pekee, ikielekeza juhudi kwa wakimbizi wapya wa Sudan. 

Hata hivyo, mwezi Aprili shirika hilo litalazimika kukata misaada yote kwa wakimbizi wapya wa Sudan. 

Kwa miezi kadhaa, wakimbizi wengi kutoka Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, na Nigeria, hawajapokea msaada wowote kutokana na ufadhili mdogo. Shirika hilo limesisitiza kuwa “Kupunguza mgao kunachochea ushindani kati ya wakimbizi, wanaorejea na jamii zinazowakaribisha juu ya rasilimali ambazo tayari ni chache, na hivyo kupanda mbegu za migogoro na ukosefu wa utulivu.”

WFP inasambaza chakula kwa wakimbizi wa Sudan wanaovuka kuelekea Chad.
© WFP/Eloge Mbaihondoum
WFP inasambaza chakula kwa wakimbizi wa Sudan wanaovuka kuelekea Chad.

Athari za changamoto ya ufadhili

Honnorat ameonya kwamba "Mchanganyiko wa sababu kutokana na mzozo nchini Sudan unazidisha ufadhili duni na uliokithiri wa hatua za kibinadamu nchini Chad. Tunahitaji wafadhili ili kuzuia hali kuwa janga la kila kitu,” 

Miezi kumi baada ya mzozo mkubwa kuzuka nchini Sudan, zaidi ya wakimbizi 559,000 wa Sudan na wakimbizi 150,000 wa Chad wamevuka na kuingia Chad, ambayo sasa inahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni moja, na kuifanya kuwa moja ya nchi zenye idadi kubwa ya wakimbizi wanaoongezeka kwa kasi zaidi barani Afrika.

Chad pia inakabiliwa na mwaka wake wa tano mfululizo wa changamoto ya chakula, huku njaa kali ikitarajiwa kuathiri watu milioni 2.9 wakati wa msimu wa muambo Juni-Agosti - ambao unaambatana na msimu wa mvua. 

Mwezi Februari, Serikali ilitangaza dharura ya chakula na lishe ikionyesha uharaka wa kuchukua hatua kuhusu hali hiyo.

Janga la wakimbizi

Kwa mujibu wa WFP wakimbizi wengi huvuka mpaka wakiwa wamebeba mzigo wakiwa na kiwewe, njaa na kuathirika visa vya kutisha vya vurugu. 

Na wanategemea msaada wa kibinadamu ili kuishi. 

Tathmini ya WFP inaonyesha kuwa ulaji wa chakula uko katika viwango duni hasa  mipakani kwa asilimia 90 ya wakimbizi wapya, asilimia 77 ya wakimbizi waliokuwepo hapo awali na asilimia 67 ya jamii zinazowahifadhi. 

Hali ya lishe pia shirika hilo linasema inatia wasiwasi hasa ambapo asilimia 40 ya watoto wakimbizi wa Sudan walio chini ya umri wa miaka mitano wanaugua tatizo la upungufu mkubwa wa damu.

"Kupunguza msaada kwa jamii zinazokabiliwa na kiwango hiki cha mazingira magumu ni jambo lisilofikirika. Tunalazimisha familia kuruka milo na kula chakula kidogo cha lishe, na hili linaweka msingi wa changamoto ya lishe, changamoto ya kukosekana kwa utulivu, na janga la watu kuhama makazi yao," ameonya Honnorat.

Ili kuhakikisha msaada unaoendelea kwa watu walioathiriwa na mgogoro nchini Chad katika kipindi cha miezi sita ijayo, WFP inahitaji haraka dola milioni 242.