Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matendo ya Taliban kuwaweka kizuizini wanawake kwa sababu ya mavazi yakome: Wataalamu wa UN

Mwanamke na mtoto wake wakipitia kambi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Afghanistan. (Picha ya maktaba)
© UNOCHA/Christophe Verhellen
Mwanamke na mtoto wake wakipitia kambi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Afghanistan. (Picha ya maktaba)

Matendo ya Taliban kuwaweka kizuizini wanawake kwa sababu ya mavazi yakome: Wataalamu wa UN

Haki za binadamu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa leo wameelezea wasi wasi wao kutokana na ripoti nyingi kwamba wanawake na wasichana wengi nchini Afghanistan wamewekwa kuzuizini kiholela na kufanyiwa vitendo viovu tangu mapema Januari mwaka huu 2024 kwa madai ya kukiuka kanuni za mavazi za Taliban kwa wanawake.

"Tunawahimiza Taliban kusitisha unyimwaji wa uhuru kiholela unaolenga wanawake na wasichana kulingana na kanuni kali za mavazi walizoweka, na kuwaachilia mara moja wanawake na wasichana ambao wanaweza kuwa bado wanazuiliwa." Wataalam hao wa Umoja wa Mataifa akiwemo Richard Bennett, Mtaalamu Maalum kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Afghanistan, wamesema.

Wametoa wito kwa mamlaka husika kuzingatia majukumu ya kimataifa Afghanistan ya haki za binadamu  ikiwa ni pamoja na chini ya Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake, na kufanya kazi kuelekea kuzingatia kanuni za haki za binadamu, kutobagua na utawala wa sheria.

Operesheni hizo hapo awali zilianza magharibi mwa Kabul, eneo lenye wakazi wengi wa Hazara, lakini zilienea kwa kasi katika maeneo mengine ya jiji, hasa maeneo yenye watu wa Tajik, na majimbo mengine, ikiwa ni pamoja na Bamiyan, Baghlan, Balkh, Daykundi na Kunduz. Kukamatwa na kuwekwa kizuizini kulifanyika katika maeneo ya umma, ikiwa ni pamoja na madukani, shule na masoko ya mitaani.

Wanawake na wasichana walichukuliwa kwa nguvu ndani ya magari ya polisi na kushutumiwa kwa kuvaa "hijab mbaya", na kuzuiliwa kwa siri, huku Taliban wakiripotiwa kudai kuwa walikuwa wamevaa nguo za rangi na za kubana kinyume na maagizo yao. Mnamo Mei 2022, waliwaamuru wanawake wote kuzingatia "hijabu inayofaa", ikiwezekana kwa kuvaa chadari (vazi jeusi lililolegea lililofunika mwili na uso) hadharani na kuwafanya jamaa wa kiume kuwajibikia kutekeleza marufuku hiyo au waadhibiwe.

"Wanawake na wasichana wameripotiwa kushikiliwa katika maeneo yenye msongamano wa watu katika vituo vya polisi, wanapokea mlo mmoja tu kwa siku, huku baadhi yao wakifanyiwa ukatili wa kimwili, vitisho na manyanyaso," wataalamu hao wamesema na kuongeza kuwa, "Uwakilishi wa kisheria na upatikanaji wa haki au fidia haukupatikana kwa wanawake hao".

Wamebainisha kuwa kuachiliwa kwa wanawake na wasichana kunategemea wanafamilia wa kiume na wazee wa jamii kutoa hakikisho, mara nyingi kwa maandishi, kwamba watazingatia kanuni za mavazi zilizowekwa katika siku zijazo.

"Mbali na kuwaadhibu wanawake kwa kile wanachovaa, kuwapa wanaume jukumu la mavazi ya wanawake kunakiuka haki ya wanawake na kuendeleza mfumo wa kitaasisi wa ubaguzi, udhibiti wa wanawake na wasichana, na unapunguza zaidi nafasi yao katika jamii," wataalam wamesema.

Pia unaweza kusoma hapa: https://news.un.org/sw/story/2024/01/1170797 

Walibainisha kuwa pamoja na baadhi ya wanawake na wasichana kuachiwa baada ya saa chache, wengine walikaa mahabusu kwa siku au wiki kadhaa na kutokana na kutokuwepo uwazi na upatikanaji wa haki, haijulikani ni wangapi ambao bado wanashikiliwa, pengine bila taarifa kuwahusu.

"Wimbi hili la sasa la kunyimwa uhuru linazuia zaidi uhuru wa kujieleza na kutembea kwa wanawake na wasichana, na linakiuka haki za binadamu na wakala wao," wataalam wamesisitiza. 

Wataalamu hao waligundua kuwa hali ya wanawake na wasichana imezorota sana tangu Taliban ilipochukua mamlaka mnamo Agosti 2021, na vikwazo vinavyoongezeka kwa elimu, ajira, kujieleza, ushirika, faragha, harakati, wakala, na ushiriki katika maisha ya umma. 

Wameshauri, "Wale waliohusika na kuweka ubaguzi huu ulioenea na wa kimfumo wanapaswa kuwajibika kwa matendo yao." walisema.