Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMA yatiwa hofu na kamatakamata ya wanawake na wasichana kwa kutovaa Hijab Afghanistan

Wanawake wawili nchini Afghanistan wakitembea karibu na msikiti wa kale kwenye jimbo la Herat
UNAMA
Wanawake wawili nchini Afghanistan wakitembea karibu na msikiti wa kale kwenye jimbo la Herat

UNAMA yatiwa hofu na kamatakamata ya wanawake na wasichana kwa kutovaa Hijab Afghanistan

Wanawake

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Misaada nchini Afghanistan UNAMA leo umesema una wasiwasi mkubwa kuhusu kukamatwa kiholela na kuzuiliwa kwa wanawake na wasichana kunakofanywa na maafisa wa serikali ya Afghanistan kwa sababu ya madai ya kutofuata kanuni za mavazi ya Kiislamu.

Tangu tarehe 1 Januari, katika majimbo ya Kabul na Daykundi, UNAMA imeandika mfululizo wa kampeni za utekelezaji wa amri ya kuvaa hijab iliyotolewa na mamlaka ya Taliban. 

Katika mji mkuu Kabul, idadi kubwa ya wanawake na wasichana wameonywa na kukamatwa pia katika jiji la Nili la jimbo la Daykundi, wanawake na wasichana pia wamezuiliwa.

Uchunguzi wa madai ya unyanyasaji

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umesema unachunguza madai ya kuwekwa kizuizini bila mawasiliano na unyanyasaji na pia unajadili masuala haya na mamlaka zenyewe. 

UNAMA pia imetoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wale wote waliozuiliwa na bila masharti yoyote.

Ikikumbukwe kwamba mnamo mwezi Mei 2022 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alielezea wasiwasi wake wakati Taliban ilipotangaza kwamba wanawake wote lazima wafunike nyuso zao hadharani na kuruhusiwa kuondoka nyumbani tu katika hali ya lazima. 

Umoja wa Mataifa umesema utaendelea kusisitiza wasiwasi huu na kushirikiana na mamlaka husika juu ya hayo yanayotokea.