Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uongozi wa Taleban unaanzisha mfumo wa ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya wanawake - Haki za binadamu UN

Wanawake na watoto wakisubiri ushauri wa kitabibu katika kliniki mjini Kandahar, Afghanistan.
© UNICEF/Alessio Romenzi
Wanawake na watoto wakisubiri ushauri wa kitabibu katika kliniki mjini Kandahar, Afghanistan.

Uongozi wa Taleban unaanzisha mfumo wa ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya wanawake - Haki za binadamu UN

Haki za binadamu

Na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu wameonya kuwa uongozi wa Taliban nchini Afghanistan unaanzisha mfumo wa ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia kwa kiwango kikubwa dhidi ya wanawake na wasichana.

Taarifa ya  kundi hilo la wataalam wa haki za binadamu kutoka Geneva Uswisi imeeleza kuwa wamekuwa wakishuhudia tangu mwezi  Agosti 2021 msururu wa hatua mbalimbali za  vikwazo ambazo zimeanzishwa tangu Taliban kutwaa madaraka nchini Afghanistan, hasa zile zinazohusu wanawake na wasichana.

Wamebainisha vikwazo hivyo vinajumuisha sera ambazo, "zinajumuisha adhabu ya pamoja kwa wanawake na wasichana zinatokana na upendeleo wa kijinsia na mila zenye madhara kwa jinsia ya kike."

Wataalamu hao pia walibainisha ongezeko la hatari zinazowakabili wanawake na wasichana  ikiwemo biashara haramu ya usafirishaji yenye lengo la kulazimisha ndoa za utotoni, unyanyasaji wa kingono pamoja na utumikishaji.

Wataalamu hao wamesisitiza wito wao kwa jumuiya za kimataifa kuongeza kasi ya misaada ya kibinadamu inayohitajika kwa watu wa Afghanistan, na kutambua haki yao ya kupona na kupata maendeleo.