Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kukengeuka kwa Taliban kuhusu elimu ya wasichana kuna athari kubwa:UN 

Wasichana katika shule ya Herat, Afghanistan.
© UNICEF/Sayed Bidel
Wasichana katika shule ya Herat, Afghanistan.

Kukengeuka kwa Taliban kuhusu elimu ya wasichana kuna athari kubwa:UN 

Haki za binadamu

Kufuatia mtafaruku wa kufungua tena shule za sekondari za wasichana nchini Afghanistan leo Jumatano, mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea kuchanganyikiwa na kusikitishwa kwake kwamba miezi sita baada ya Taliban kunyakua mamlaka, wasichana wa shule za upili bado hawajarejea darasani. 

"Kushindwa kwa mamlaka husika kuzingatia ahadi za kufungua tena shule za wasichana zaidi ya darasa la sita licha ya ahadi za mara kwa mara kuhusu elimu ya wasichana, ikiwa ni pamoja na wakati wa ziara yangu Kabul wiki mbili zilizopita ni zahma kubwa kwa Afghanistan", amesema kamishna mkuu. Michelle Bachelet katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis. 

Amesisitiza kuwa kunyimwa elimu kunakiuka haki za binadamu za wanawake na wasichana. 

Wasiwasi mkubwa 

Ingawa shule za upili zilipangwa kufungua milango kwa wasichana kote nchini, mamlaka ya Taliban iliripotiwa kutengua hatua hiyo mapema leo Jumatano, ikisubiri uamuzi uliotolewa kuhusu sare wanazopaswa kuvaa. 

"Kunyimwa elimu kunakiuka haki za binadamu za wanawake na wasichana dhidi ya haki yao sawa ya kupata elimu, na pia kunatoa mwanya zaidi katika suala la unyanyasaji, umaskini na unyonyaji," Bi. Bachelet ameelezea. 

Nakumbuka niliyoshuhudia 

Akikumbuka ziara yake ya hivi majuzi huko Kabul ambapo wanawake walisisitiza kwamba wanataka kuzungumza na Taliban wenyewe. 

Bi. Bachelet amesema wanawake hao walimwambia kwamba wana "Taarifa, suluhu na uwezo wa kusaidia kupanga njia ya kuondokana na mgogoro huu wa kiuchumi, kibinadamu na haki za binadamu nchini Afghanistan.Walisisitiza juu ya haki sawa ya elimu bora katika ngazi ya msingi, sekondari na elimu ya juu na walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kufunguliwa kwa shule leo". 

Ubaguzi wa kimuundo 

Wakati raia wa Afghanistan wakikabiliwa na athari za migogoro mingi inayoingiliana, afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa  ameelezea uamuzi huo ni wa kutia wa wasiwasi mkubwa. 

"Kukatisha tamaa nusu ya idadi ya watu wa Afghanistan hakuna tija na sio haki," Bi Bachelet amesema, akiongeza kuwa "ubaguzi wa kimuundo kama huu pia unaharibu sana matarajio ya nchi ya kujikwamua na maendeleo ya siku zijazo." 

Ametoa wito kwa Taliban "kuheshimu haki zote za elimu za wasichana na kufungua shule kwa wanafunzi wote bila ubaguzi au kucheleweshwa zaidi". 

Matumaini yaliyovunjika 

Naye mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Catherine Russell, pia ametoa taarifa akielezea uamuzi huo kama "kikwazo kikubwa kwa wasichana na mustakabali wao". 

Amesema "Mamilioni ya wasichana wa shule za sekondari kote Afghanistan wameamka wakiwa na matumaini leo kwamba wataweza kurejea shuleni na kuendelea na masomo,"  

Haikuchukua muda kwa matumaini yao kuzimwa. 

Kulingana na Bi. Russell uamuzi huo unamaanisha kwamba kizazi kizima cha wasichana balehe au vigori “kinanyimwa haki yao ya kupata elimu na kunyimwa fursa ya kupata ujuzi wanaohitaji ili kujenga maisha yao ya baadaye.” 

Amezitaka mamlaka husika kuheshimu dhamira yao ya elimu ya watoto wa kike bila kuchelewa tena na kuwataka viongozi wa jamii katika kila kona ya nchi hiyo kuunga mkono elimu ya wasichana. 

"Watoto wote wanastahili kuwa shuleni. Hii ndiyo njia ya uhakika ya kuiweka nchi katika mkono unaofaa na wa uhakika kuelekea amani na ustawi ambao watu wa Afghanistan wanastahili,” amesema mkuu huyo wa UNICEF. 

Tunalaani uamuazi huo:UNAMA 

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan (UNAMA) umetoa hisia zake kuhusu habari hiyo, kwa kutuma ujumbe kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba "unasikitishwa na tangazo lililoripotiwa leo na Taliban kwamba wanaongeza zaidi marufuku yao ya muda usiojulikana kwa wanafunzi wa kike wanaosoma zaidi ya darasa la 6 kuruhusiwa kurejea shuleni. Na hivyo wanalaani tangazo nah atua hiyo”. 

Nimesikitishwa na uamuzi wa Taliban:Guterres 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiongeza sauti yake katika uamuzi huo wa Taliban amesema “Nimesikitishwa sana na tangazo la mamlaka ya Taliban nchini Afghanistan kwamba elimu ya wasichana kutoka darasa la sita imesimamishwa tena hadi ilani nyingine itakapotolewa.” 

Ameongeza kuwa kuanza kwa mwaka mpya wa shule kumetarajiwa na wanafunzi wote, wasichana na wavulana, na wazazi na familia.  

Hivyo “Kushindwa kwa mamlaka  kuuhakikisha kufungua tena shule za wasichana walio zaidi ya darasa la sita, licha ya kuahidi mara kwa mara, ni jambo la kutamausha na kuleta madhara makubwa kwa Afghanistan.”Amesema Guterres  

Ameongeza kuwa “Kunyimwa elimu sio tu kwamba kunakiuka haki sawa za wanawake na wasichana kupata elimu, pia kunahatarisha mustakabali wa nchi kwa kuzingatia michango mikubwa ya wanawake na wasichana wa Afghanistan. Ninatoa wito kwa mamlaka ya Taliban kufungua shule kwa wanafunzi wote bila kuchelewa zaidi.”