Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taliban: Marufuku kwa wanawake na wasichana inagharimu uhalali wenu nyumbani na nje ya nchi - Mkuu UNAMA

Kundi la wanawake na watoto linatembea kwenye barabara yenye vumbi katika eneo lenye milima na ukame nchini Afghanistan, huku jengo likiwa nyuma yake.
© UNICEF/Mark Naftalin Kundi la wanawake na watoto wao wakitembea Daikundi katika eneo la mbali la katikati mwa Afghanistan.

Taliban: Marufuku kwa wanawake na wasichana inagharimu uhalali wenu nyumbani na nje ya nchi - Mkuu UNAMA

Haki za binadamu

Vizuizi vingi vilivyowekwa kwa wanawake na wasichana na watawala wa Afghanistan vinawagharimu Taliban "uhalali wa ndani na wa kimataifa" na havipendwi nchini kote, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Roza Otunbayeva amesema hayo akitoa taarifa kwa Baraza la Usalama kuhusu hali mbaya inayoikabili nchi hiyo na juhudi za kimataifa za misaada, huku wafanyakazi wanawake wa Umoja wa Mataifa wakiwa miongoni mwa wale ambao sasa wamezuiwa na amri zao. 

"Hatutaweka wafanyakazi wetu wa kitaifa hatarini na kwa hivyo tunawaomba wasiripoti ofisini," amesema, akiongeza kuwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan (UNAMA) anaouongoza pia, hauna nia ya kujaza nafasi za wanawake hao kwa kuleta wafanyakazi wa kiume.  

Hakuna hakikisho 

Amesema Taliban hawakumpa maelezo yoyote kuhusu marufuku hiyo, "na hakuna hakikisho kwamba itaondolewa." 

Ameeleza kwamba wakati Taleban wanaendelea na uminyaji wa haki za binadamu kwa wanawake na wasichana, "ni vigumu sana kwamba serikali yao itambulike". 

Nusu ya watu wanateseka 

Amesema kutokana na ushirikiano wa UNAMA na mashirika ya kiraia nchini kote: "Pia ni wazi kwamba amri hizi hazikubaliki sana miongoni mwa wakazi wa Afghanistan. Zinagharimu Taliban uhalali wa ndani na kimataifa huku wakileta mateso kwa nusu ya watu wao na kuharibu uchumi."

Mkuu huyo wa UNAMA ametoa wito kwa mabalozi na jumuiya ya kimataifa kufanya zaidi ili kuhakikisha uthabiti wa siku za usoni wa uchumi wa Afghanistan, hasa kutokana na kupungua kwa ufadhili wa kibinadamu unaotarajiwa mwaka huu. 

Katika maeneo mengine yanayotia wasiwasi, mkuu huyo wa UNAMA amesema licha ya juhudi za pamoja za kukabiliana na ugaidi, kundi la kigaidi la ISIL-KP linaendelea kuwalenga maafisa wa Taliban na raia. 

Ingawa unyakuzi wa Taliban umesababisha kupungua kwa kasi kwa vifo vya raia, amesema Huduma ya Umoja wa Mataifa ya Uteguaji Mabomu inaripoti kuwa kunaendelea kuwa na majeruhi wapatao 100 kwa mwezi kutokana na vilipuzi ambavyo vilibaki kwenye mazingira bila kulipuka. 

Akihitimisha ameliambia Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba UNAMA na mfumo wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan utaendelea kuwahusisha Wa Taliban, wakijenga "njia zilizowekwa za kuaminika za kufanya kazi". 

"Tunaweza kufanya mengi zaidi, ikiwa Taliban itabatilisha vikwazo vyake vya kuwaadhibu wanawake."