Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Vita ikishika kasi, uchunguzi wa madai dhidi ya UNRWA ukiendelea, wito watolewa wagaza waendelee kusaidiwa

Mjini Gaza watoto wakisubiri kupokea chakula wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea
© UNDP PAPP/Abed Zagout
Mjini Gaza watoto wakisubiri kupokea chakula wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea

GAZA: Vita ikishika kasi, uchunguzi wa madai dhidi ya UNRWA ukiendelea, wito watolewa wagaza waendelee kusaidiwa

Amani na Usalama

Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa leo yameonya kwamba wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea kushika kasi Gaza kwa njia ya anga, ardhini na baharini hususan katika mji wa Kusini wa Khan Younis, makazi ya wakimbizi wa ndani yamejaa pomoni mara nne ya uwezo wake na chakula hakitoshi. 

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X zamani ukijulikana kama Twitter shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema “Kwa kweli hakuna chakula cha kutosha na picha kutoka mji mwingine kaskazini kidogo kwa Gaza wa Deir-al-Balah, zinaonyesha watu wakiwa kwenye foleni katika mvua na baridi kali kwa ajili ya kusubiri misaada.”

Katika taarifa yake ya hivi karibuni, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, imeripoti mapigano makali huko Khan Younis karibu na hospitali mbili ya Nasser ambako wagonjwa wengi waliojeruhiwa hawana njia ya kupata matibabu huku kukiwa na mapigano makali na mabomu likinukuu madakrati wasio na mipaka au Médecins Sans Frontières na hospital ya Al Amal ambako Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina PRCS, imeripoti kuendelea kwa mashambulizi ya mabomu katika maeneo ya karibu na hospital hiyo.

Pia kumekuwa na ripoti za Wapalestina wanaokimbilia kusini kuelekea Rafah mji "ambao tayari umefurika watu wengi, licha ya kukosekana kwa njia salama", limesema shirika la OCHA huku likibaini pia kuendelea kuwepo kwa ufyatuaji wa maroketi kutoka Gaza kuelekea kusini mwa Israel.

Msichana aliyetawanywa na machafuko katika makazi ya Deir Al Balah  Gaza
UN News.
Msichana aliyetawanywa na machafuko katika makazi ya Deir Al Balah Gaza

Uchunguzi wa madai dhidi ya UNRWA

Huku kukiwa na madai mazito kwamba wafanyakazi kadhaa walishirikiana na Hamas wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7 dhidi ya Israel, UNRWA imeisisitiza kwamba itafanya "kila liwezekanalo kuendelea kuwasaidia Wagaza, kama shirika kubwa zaidi la misaada katika eneo hilo.”

Uchunguzi tayari umeanzishwa na chombo cha juu zaidi cha uchunguzi cha Umoja wa Mataifa  ambacho ni Ofisi ya Huduma za Uangalizi wa Ndani OIOS wakati Jumapili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisisitiza kwamba mfanyakazi yeyote wa Umoja wa Mataifa anayehusika "katika vitendo vya ugaidi atawajibishwa".

Kati ya watu 12 wanaodaiwa kuhusika, tisa walitambuliwa mara moja na kandarasi zao zilikatishwa na UNRWA. 

Mfanyikazi mmoja alithibitishwa kufariki dunia na utambulisho wa wawili waliosalia unafanyiwa kazi.

Tarehe 17 Januari tathimini kamili na huru ya shirika hilo pia ilitangazwa na Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini.

Wakati huo huo, Bw. Guterres ametoa wito kwa nchi zilizositisha ufadhili kwa UNRWA kufikiria upya maamuzi yao, angalau kuhakikisha kuendelea kwa shughuli zake muhimu za kibinadamu.

Wafanyakazi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNOCHA, walitembelea hospitali ya Al-Aqsa huko Gaza na kuripoti kuona idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa wakiletwa kwa matibabu ya haraka, kufuatia mlipuko.
WHO Video
Wafanyakazi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNOCHA, walitembelea hospitali ya Al-Aqsa huko Gaza na kuripoti kuona idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa wakiletwa kwa matibabu ya haraka, kufuatia mlipuko.

Njaa inatanda

Akiunga mkono wito huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema katika chapisho la ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X siku jana Jumapili kwamba kukata ufadhili kwa UNRWA "kutawaumiza tu watu wa Gaza".

Ambao amesema wanakabiliwa na tishio kubwa linalonyemelea la njaa, magonjwa na kufurushwa makwao baada ya karibu miezi minne ya mashambulizi ya Israel, yaliyochochewa na mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200 na zaidi ya watu 250 kuchukuliwa mateka.

Mkuu wa UNRWA Bwana Lazzarini ameonya kwamba “Zaidi ya watu milioni mbili huko Gaza wanategemea shirika hilo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuishi lakini operesheni yake ya kibinadamu inaporomoka.”

UNRWA ina wafanyakazi 13,000 wanaohudumia jamii za Wapalestina huko Gaza. Leo takriban 3,000 wanaendelea kufanya kazi katika eneo la vita, lililopewa jukumu la kuendesha makazi kwa zaidi ya watu milioni moja, kutoa chakula na huduma za afya kwa raia walio na uhitaji mkubwa tangu kuanza kwa vita.

Hadi sasa, zaidi ya watu 26,420 wameuawa huko Gaza tangu Oktoba 7, lilisema shirika OCHA ofisi ya eneo linalokaliwa la Wapalestina la Gaza , likinukuu takwimu kutoka kwa wizara ya afya ya Gaza. 

Takriban wanajeshi 1,269 wa Israel pia wameuawa katika mapigano hayo, kwa mujibu wa jeshi la Israel.

"Watu wa Gaza wamekuwa wakivumilia hali ya kutisha na kunyimwa vitu kwa miezi kadhaa sasa" amesema afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya dharura Martin Griffiths jana Jumapili kupitia ukurasa wake wa X na kuongeza kuwa  "Mahitaji yao hayajawahi kuwa juu zaidi  kama sasa na uwezo wetu wa kibinadamu wa kuwasaidia haujawahi kuwa chini ya hali kama hiyo ya tishio. Tunahitaji kujiongeza kikamilifu ili kuwapa watu wa Gaza muda wa matumaini."