Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wiki 10 za jinamizi kwa watoto Gaza: UN

Watoto wakiangalia nyumba yao iliyosambaratishwa kwenye mji wa Rafah Kusini mwa Gaza
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto wakiangalia nyumba yao iliyosambaratishwa kwenye mji wa Rafah Kusini mwa Gaza

Wiki 10 za jinamizi kwa watoto Gaza: UN

Amani na Usalama

Ukanda wa Gaza huko Mashariki ya Kati ni mahali pa hatari zaidi duniani kuwa mtoto na vifo vya vijana kutokana na maradhi huenda vikapita vile vya mashambulizi ya mabomu bila kuwepo kwa usitishaji mapigano, limeonya leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.

Ukosefu wa chakula, maji, makazi na usafi wa mazingira unaendelea kuweka maisha ya watoto hatarini huku wakiteseka chini ya mashambulizi ya anga bila mahali salama pa kwenda, amesema msemaji wa UNICEF James Elder, ambaye hivi karibuni amerejea kutoka katika eneo hilo.

Kabla ya mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unaotarajiwa kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ili kuwezesha upatikanaji wa misaada, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba "kila mtoto Gaza amepitia hizi wiki 10 za hali ya jrehanamu na hakuna hata mmoja wao anayeweza kutoroka".

Ameongeza kuwa "Mmoja wa mzazi wa mtoto aliyekuwa mgonjwa mahututi aliniambia, hali yetu ni taabu tupu sijui kama tutafanikiwa katika hili," amesema.

Kwa mujibu wa mamlaka za afya Gaza, zaidi ya Wapalestina 19,400 wameuawa katika eneo hilo tangu kuanza kwa Israel kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya kigaidi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba, karibu asilimia 70 kati yao wakiwa wanawake na watoto.

Zaidi ya Wapalestina 52,000 wamejeruhiwa na upatikanaji wa huduma za kuokoa maisha ni mdogo sana. 

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema leo kwamba ni hospitali nane tu kati ya 36 katika Ukanda huo ambazo angalau zinafanya kazi kwa kiasi fulani.

Watoto wanaohifadhiwa katika shule ya UNRWA huko Gaza wakifurahia mkate unaosambazwa na WFP.
© WFP/Ali Jadallah
Watoto wanaohifadhiwa katika shule ya UNRWA huko Gaza wakifurahia mkate unaosambazwa na WFP.

Hali ni ya kusikitisha na kushangaza

Kwa mujibu wa James Elder, “Hospitali zimefurika watoto na wazazi wao, wote wakiwa na vidonda vya kutisha  kutokana na vita”. 

Amesisitiza kuwa akiwa Ukanda huo alikutana na vijana wengi waliokatwa viungo. Takriban watoto 1,000 huko Gaza wamepoteza mguu mmoja au yote miwili, amesema.

Msemaji wa WHO Dk. Margaret Harris ameongeza kuwa wafanyakazi wa WHO huko Gaza wamezungumzia juu ya kutoweza hata kutembea katika wodi za dharura "kwa hofu ya kukanyaga watu waliolala chini wakiwa katika maumivu makali na kuomba chakula na maji.”

Ameiita hali hiyo "isiyofaa" na kusema kwamba "Huwezi kuamini kwamba ulimwengu unaruhusu hii kuendelea".

Hospitali yapigwa makombora

Katika muda wa saa 48 zilizopita, hospitali kubwa zaidi iliyosalia ikifanyakazi huko Gaza, Hospitali ya Al Nasser kwenye mji wa Khan Younis Kusini mwa Gaza imepigwa makombora mara mbili, amesema Bwana Elder.

Hospitali hiyo "sio tu inahifadhi idadi kubwa ya watoto ambao tayari wamejeruhiwa vibaya katika mashambulizi majumbani kwao, lakini mamia ya wanawake na watoto wanaotafuta usalama", amesisitiza, akimaanisha wale ambao wamelazimika kukimbia kwa sababu ya uhasama na kuhamishwa kutokana na maagizo ya jeshi la Israel.

Takriban watu milioni 1.9, au idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo, wanakadiriwa kuyahama makazi yao huko Gaza.

Watoto waliojeruhiwa wanaokabiliana na kupoteza wapendwa wao wamelazimika kuhama tena na tena, amesema Elder. 

Na kuongeza kuwa "Watoto na familia zao wanaenda wapi? Hawako salama hospitalini wala si salama katika makazi ya muda na kwa hakika hawako salama katika maeneo yanayoitwa salama”.

Shule ya UNRWA ya Nuseirat katikati mwa Gaza imegeuka kuwa makazi ya dharura kwa maelfu ya watu waliofurushwa makwao
UN News/Ziad Taleb
Shule ya UNRWA ya Nuseirat katikati mwa Gaza imegeuka kuwa makazi ya dharura kwa maelfu ya watu waliofurushwa makwao

Hakuna mahali palipo salama

Msemaji wa UNICEF ameeleza kuwa "maeneo salama yamekuwa kitu kingine chochote ila salama kwa sababu yameteuliwa kwa upande mmoja Israel pekee na yanakosa "rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuishi kama chakula, maji, dawa, ulinzi.”

Bwana Elder ameyataja maeneo hayo kuwa ni “vipande vidogo vya ardhi isiyo na maji, au kona za barabara, ni majengo yasiyokamilika, yasiyo na maji, hakuna vifaa, hakuna mahali pa kujikinga na baridi na mvua na hakuna usafi wa mazingira”.

"Chini ya hali ya sasa ya kuzingirwa, vifaa vya kutosha kwa maeneo kama haya haviwezekani," amesema, akiongeza kuwa wakati ziara yake hivi karibuni huko Gaza alishuhudia ukweli huu moja kwa moja.

Kuhara na utapiamlo

Msemaji huyo wa UNICEF ameangazia hali mbaya ya ukosefu wa vyoo vya kutosha, akiashiria kwamba huko Gaza choo kimoja kinatumika na watu 700 kwa wastani. Kesi za kuhara kwa watoto ni zaidi ya 100,000 na pamoja na kuongezeka kwa utapiamlo kunaweza kuwa kubaya zaidi.

Bwana Elder ameongeza kuwa zaidi ya watoto 130,000 walio chini ya umri wa miaka miwili hawapati "kunyonyesha maziwa ya mama yenye kuokoa maisha na lishe ya nyongeza inayolingana na umri kama vile virutubisho vinavyohitajika.”

Wafanyakazi wa WHO walishiriki katika msafara wa pamoja wa UN kwenye hosptali ya Al-Shifa kwa ajili ya kupeleka vifaa ya matibabu na kuona hali halisi.
WHO
Wafanyakazi wa WHO walishiriki katika msafara wa pamoja wa UN kwenye hosptali ya Al-Shifa kwa ajili ya kupeleka vifaa ya matibabu na kuona hali halisi.

Kusitisha mapigano ndio njia pekee

Utoaji wa misaada ni "suala la maisha au kifo kwa watoto huko Gaza” amesema Bwana Elder, akiongeza kuwa na masharti ya kutoa msaada huo hayafikiwi.

Idadi ya malori ya misaada yanayoruhusiwa kuingia Gaza bado "chini ya wastani wa kila siku wa malori ya mizigo 500" ambayo yaliingia kila siku ya kazi kabla ya Oktoba 7, kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu, OCHA

Siku ya Jumapili, OCHA ilisema kwamba malori 102 yaliyobeba vifaa vya kibinadamu na malori manne ya mafuta yaliingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah kutoka Misri na malori mengine 79 yaliingia kupitia kivuko cha Kerem Shalom kutoka Israel, kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ongezeko hilo la machafuko.

Dkt. Harris wa WHO amesisitiza kwamba mbali ya kupeleka vifaa kuvuka mpaka ndani ya eneo hilo, ilikuwa ni changamoto kupata msaada pale inapohitajika, kwa sababu ya uhasama unaoendelea lakini pia uharibifu mkubwa wa barabara.

"Usitishaji mapigano wa haraka na wa muda mrefu wa kibinadamu ndiyo njia pekee ya kukomesha mauaji na kujeruhiwa kwa watoto, na vifo vya watoto kutokana na magonjwa, na kuwezesha utoaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu inayohitajika sana ya kuokoa maisha," amesema Bwana Elder.