Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: WHO yataka fursa kufikisha huduma muhimu hospitali ya Nasser

Mwanamume akiwapikia watoto wake chakula kwenye moto wa kuni mbele ya nyumba yake iliyoharibiwa katika kitongoji cha al-Rimal, magharibi mwa Jiji la Gaza.
© UNICEF/Omar Al-Qattaa
Mwanamume akiwapikia watoto wake chakula kwenye moto wa kuni mbele ya nyumba yake iliyoharibiwa katika kitongoji cha al-Rimal, magharibi mwa Jiji la Gaza.

Gaza: WHO yataka fursa kufikisha huduma muhimu hospitali ya Nasser

Amani na Usalama

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Ulimwenguni WHO leo limeomba fursa ya ufikiaji wa hospitali ya Nasser ili kutoa huduma muhimu na limeelezea wasiwasi mkubwa juu ya uvamizi wa vikosi vya Israeli kwenye hospitali ya Khan Younis, kusini mwa Gaza.

Jeshi la Israel lilitangaza jana Alhamisi kuwa lilikuwa likifanya operesheni maalum na yenye mipaka katika hospitali ya Nasser, iliyoko Khan Younis. 

Hiyo ni hospitali kubwa zaidi kusini mwa Gaza. Na kwa mujibu wa WHO, uvamizi wa kijeshi kwenye kituo cha matibabu cha Nasser na ripoti zinazotoka hospitalini zinatisha sana.

Shirika hilo la WHO linahofia usalama wa wagonjwa, wafanyakazi wa afya na raia wanaohifadhiwa hospitalini na linatoa wito wa kulindwa kwa huduma za afya na kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu.

"Wagonjwa, wafanyikazi wa afya na raia wanaotafuta hifadhi wanastahili kuwa salama na sio hatarini katika maeneo ya huduma za afyai," amesema Tarik Jasarevic, msemaji wa WHO.

Uharaka wa kufikisha mafuta

Katika eneo hilo WHO inajaribu kuifikiaji hospitali ya Nasser, wakati wanajeshi wa Israeli wakiendelea na uvamizi wao kwenye eneo ambalo maelfu ya raia wamenaswa. 

Shirika hilo linasema lina wasiwasi kuhusu hatima ya "waliojeruhiwa vibaya na wagonjwa ambao bado wako ndani ya hospitali".

Tarik Jasarevic ameongeza kuwa “Kuna hitaji la dharura la kupeleka mafuta ili kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea. Tunajaribu kufikia hospitali kwa sababu watu ambao bado wako katika kituo hicho cha matibabu cha Nasser wanahitaji msaada”.

Kulingana na duru za habari, vikosi vya Israeli vilivamia Hospitali ya Nasser, kituo kikubwa zaidi cha huduma za afya katika eneo hilo, jana Alhamisi. 

Shambulio hilo lilikuja baada ya kuzingirwa kwa wiki moja, ambapo hospitali hiyo ilinyimwa chakula, mafuta na vifaa vya matibabu.

Waliwalazimisha watu waliokimbia makazi yao na familia za wafanyikazi wa huduma za afya waliohifadhiwa hospitalini kukimbia.

Kulingana na WHO, kitengo cha mifupa cha hospitali ya Nasser hakifanyi kazi, na kuripotiwa uharibifu wa kitengo cha mifupa kumepunguza zaidi uwezo wake wa kutoa huduma ya dharura.

Muhimili wa mfumo wa afya kusini mwa Gaza

"Kuendelea kuzorota kwa taasisi hiyo kunamaanisha kupoteza maisha zaidi, magonjwa na mateso," limeonya shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa lenye makao yake makuu mjini Geneva, likibainisha kuwa "hospitali hiyo ni uti wa mgongo wa mfumo wa afya kusini mwa Ukanda wa Gaza.”

Kwa WHO, hospitali ya Nasser lazima iendelee kufanya kazi. Hasa kwa vile taasisi za afya kusini mwa Gaza "hazina uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi". Miundombinu hii ya afya "tayari inafanya kazi zaidi ya uwezo wake wa juu kwa zaidi ya karibu asilimia 350 ya vitanda na zaidi ya asilimia 240 ya vitanda katika vitengo vya wagonjwa mahututi".

Awali WHO ilisema ilishtushwa na ripoti za kulazimishwa kwa wagonjwa wengi kuhamishwa hadi jengo lingine. 

WHO imeonya mara kwa mara kwamba kuwanyima wagonjwa huduma ya kuokoa maisha na kulazimisha harakati za wagonjwa na waliojeruhiwa kuhama kunaweza kusababisha kuzorota zaidi kwa afya au hata vifo.

"Afya ya mgonjwa lazima iwe kipaumbele na huduma zisizokatizwa katika mazingira salama lazima uhakikishwe," amesisitiza Tarik Jasarevic, msemaji wa WHO na kuongeza kuwa "Waliojeruhiwa vibaya na wagonjwa wamesalia hospitalini”. 

Zaidi ya hayo amesema tathmini za matibabu zinahitajika ili kutambua wagonjwa muhimu zaidi na kuwezesha uhamisho wao kwa njia salama.

Hospitali hazipaswi kuwa za kijeshi au kushambuliwa

WHO inakumbusha kwamba Umoja wa Mataifa unashirikiana na mamlaka ya Israel kupata fursa ya ufikiaji hospitali hiyo haraka. 

"Hospitali hazipaswi kuwa za kijeshi au kushambuliwa," amesema msemaji huyo, akikumbusha kuwa sheria za kimataifa za kibinadamu na kanuni za tahadhari na uwiano lazima ziheshimiwe.

Ikumbukwe kwamba jana Alhamisi, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu OHCHR, pia ilielezea wasiwasi mkubwa. Ikisema "Uvamizi huu unakuja baada ya kuzingirwa kwa wiki nzima ambako kulikatiza usambazaji wa dawa, chakula na mafuta," kwa mujibu wa msemaji wa OHCHR Ravina Shamdasani katika taarifa yake kwa vyombo vya habari. 

Msemaji huyo ameonya kwamba uvamizi huo unaonekana kuwa sehemu ya mfululizo wa mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya Israel dhidi ya miundombinu ya raia muhimu kwa uhai wa Gaza, hasa hospitali.

Kwa upana zaidi, amesema wahudumu wa kibinadamu na wa afya wanaendelea kukabiliwa na changamoto na hatari kubwa katika kuwahudumia watu wanaohitaji msaada wa haraka na kuokoa maisha, hasa kutokana na kuendelea kwa mashambulizi kwenye vituo vya afya, ukosefu wa vifaa na msongamano wa watu.

Kati ya Oktoba 7 mwaka jana na Februari 12 mwaka huu, kulikuwa na karibu mashambulizi 380 dhidi ya huduma za afya katika Ukanda wa Gaza, na kuathiri karibu vituo 100 vya afya na karibu magari 100 ya wagonjwa, kulingana na takwimu za WHO. 

Theluthi mbili ya mashambulizi haya yaliripotiwa katika majimbo ya Gaza na Gaza Kaskazini.