Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa ufupi: Mauaji ya mlinda amani CAR; Kipindupindu; Matumizi ya tumbaku

UN Photo/Catianne Tijerina
UN Photo/Catianne Tijerina
UN Photo/Catianne Tijerina

Habari kwa ufupi: Mauaji ya mlinda amani CAR; Kipindupindu; Matumizi ya tumbaku

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani mauaji ya jana Januari 15 ambapo aliuawa mlinda amani mmoja wa kutoka Cameroon aliyekuwa anahudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) na kujeruhiwa kwa watu wengine watano, wawili kati yao wakiwa wamejeruhiwa mno kutokana na mlipuko huko Mbindali, katika Mkoa wa Ouham-Pendé, kaskazini-magharibi mwa Paoua. 

Msemaji wa Katibu Mkuu kupitia taarifa aliyoitoa usiku wa kuamkia leo kwa saa za New York amesema Guterres anatoa wito kwa mamlaka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kutoacha juhudi zozote katika kuwabaini wahusika wa shambulio hili na kuwafikisha mahakamani haraka. 

Wagonjwa wa kipindupindu wameongezeka kwa kasi Afrika mwanzoni mwa mwaka 2023
© WHO
Wagonjwa wa kipindupindu wameongezeka kwa kasi Afrika mwanzoni mwa mwaka 2023

Afya

Huku visa vya kipindupindu vikizidi kuongezeka katika maeneo ya Kusini mwa Afrika, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linataka kuzingatiwa zaidi kwa watoto katika kukabiliana na kipindupindu. Janga la kipindupindu ambalo liliathiri nchi nyingi za Mashariki na Kusini mwa Afrika mwaka 2023 linaendelea kuathiri eneo hilo, na kuweka matatizo ya ziada kwa jamii na vituo vya afya. 

Tangu mwaka jana 2023, nchi 13 katika kanda hiyo zimepambana na milipuko mibaya zaidi ya kipindupindu kuwahi kukumba eneo hilo kwa miaka mingi, na kufikia jana Januari 15, 2024, zaidi ya wagonjwa 200,000, pamoja na vifo zaidi ya 3,000, vimeripotiwa. 

Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kuwa idadi ya wanaotumia tumbaku inapungua, ikionyesha mabadiliko makubwa katika janga la tumbaku ulimwenguni. (Maktaba)
Unsplash/Ali Yahya
Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kuwa idadi ya wanaotumia tumbaku inapungua, ikionyesha mabadiliko makubwa katika janga la tumbaku ulimwenguni. (Maktaba)

Tumbaku

Na matumizi ya tumbaku yanaoekana kupungua licha ya juhudi za sekta ya tumbaku kuhatarisha maendeleo, imeeleza ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO. WHO inaeleza kwamba mienendo ya kuanzia mwaka 2022 inaonesha takriban mtu mzima 1 kati ya 5 duniani kote anatumia tumbaku ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2000 ambapo ilikuwa ni mtu 1 kati ya 3. 

WHO inazitaka nchi kuendelea kuweka sera za kudhibiti tumbaku na kuendelea kupambana dhidi ya sekta ya tumbaku kuingilia hatua hizi.