Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya tumbaku yamepungua, uwekezaji utanusuru watu wengi zaidi:WHO

Shirika la Afya Ulimwenguni linaongeza ufahamu juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku na uvutaji wa moshi wa sigara.
Unsplash/Kristaps Solims
Shirika la Afya Ulimwenguni linaongeza ufahamu juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku na uvutaji wa moshi wa sigara.

Matumizi ya tumbaku yamepungua, uwekezaji utanusuru watu wengi zaidi:WHO

Afya

Ripoti mpya ya mwenendo wa matumizi ya tumbaku iliyotolewa leo na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO inaonesha idadi ya watumiaji wa bidhaa za tumbaku duniani imepungua kwa zaidi ya watu milioni mbili tangu mwaka 2015 na inatarajiwa kupungua zaidi ifikapo mwaka 2025.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya nne ya mwenendo wa matumizi ya bidhaa za tumbani duniani, mwaka 2015 watumiaji walikuwa bilioni 1.32 na sasa ni bilioni 1.30 huku ifdadi hiyo ikitarajiwa kushuka hadi bilioni 1.27 ifikapo mwaka 2025. 

Nchi 60 zimetajwa kuwa mbioni kutimiza lengo la hiyari la kimataifa la kupunguza kwa asilimia 30 matumizi ya tumbaku kati yam waka 2010 na 2025 ikiwa ni ongezeko kutoka nchi 32 miaka miwili iliyopita. 

WHO imesema maisha ya mamilioni ya watu yameokolewa kwa kuwa na sera madhubuto na zenye ufanisi za kudhibiti matumizi ya bidhaa za tumbaku chini ya mkakati wa WHO FCTC na MPOWER na hayani mafanikio makubwa katika vita dhidi ya uraibu wa tumbaku. 

Akizungumzia mafanikio hayo mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedross Adhanom Ghebreyesus anesema “Inatia moyo sana kuona kwamba watu wachache wanatumia bidhaa za tumbaku kila mwaka na nchi nyingi ziko mbioni kufikia malengo ya kimataifa.Hata hivyo bado safari bado ni ndefu na makampuni ya tumbaku yataendelea kutumia kila mbinu kutetea faida kubwa wanayoipata kwa kuuza bidhaa hizo hatari. Tunazichagiza nchi zote kutumia nyenzo bora zilizopo kusaidia watu kuacha matumizi ya tumbaku na kuokoa maisha.” 

Ripoti pia imezitaka nchi kusongesha mchakato wa utekelezaji wa hatua zilizoorodheshwa kwenye makakati wa WHO wa FCTC ili kuendelea kupunguza idadi ya watu walio hatarini kuugua au kufa kutokana na magonjwa  yanayochangiwa na matumizi ya tumbaku.

Naye Dkt. Ruediger Krech mkurugenzi wa WHO idara ya kuchagiza afya amesema “Ni bayana kwamba udhibiti wa matumizi ya tumbaku una tija na tunawajibu wa kimaadili kwa watu wetu kusongesha jitihada ili kutimiza malengo ya maendeleo endelevu . Pamoja na mafanikio bado tunahitaji juhudi zaidi.” 

WHO inasema kuwa matumizi ya afya duniani na upotevu wa tija kutokana na matumizi ya tumbaku ni sawa na $1.4 trilioni kila mwaka.
Unsplash/Mathew MacQuarrie
WHO inasema kuwa matumizi ya afya duniani na upotevu wa tija kutokana na matumizi ya tumbaku ni sawa na $1.4 trilioni kila mwaka.

Hali halisi  

Ripoti imebaini kwamba kwa mwaka 2020 asilimia 22.3 ya watu wote duniani walitumia bidhaa za tumbaku, asilimia 36.7 kati yao ni wanaumee na asilimia 7.8 wanawake. 

Kwa upande wa watoto ripoti imesema kuwa “takriban asilimia 38 ya Watoto wa umri wa miaka kati ya 13-15 hivi sasa wanatumia bidhaa za tumbaku milioni 13 wakiwa ni wasichana na milioni 25 wavulana.” 

Katika nchi nyingi WHO inasema ni haramu kwa watoto kununua bidhaa za tumbaku na lengo ni kuhakikisha dunia inakomesha kabisa matumizi ya tumbaku kwa watoto. 

Mwanamke akivuta sigara
Unsplash/Fotografierende
Mwanamke akivuta sigara

Mwenendo wa matumizi 

Kwa ujumla ripoti inasema punguzo la kiasi kikubwa la matumizi linashuhudia katika nchi za Amerika ambako kiwango kimeshuka kutoka asilimia 21 mwaka 2010 hadi asilimia 16 mwaka 2020. 

Nako barani Afrika ndiko kuliko na kiwango cha chini zaidi cha matumizi ya bidhaa za tumbaku ambapo mwaka 2015 watumiaji walikuwa asilimia 15 na mwaka 2020 miaka 10 baadaye kiwango kimeshuka hadi asilimia 10. 

Na barani Ulaya imeelezwa kuwa wanawake ndio watumiaji wakubwa wa bidhaa za tumbaku asilimia 18% zaidi ukilinganisha na kanda zingine .