Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iwajibisheni sekta ya tumbaku kwa uharibifu wa mazingira na afya ya binadamu:WHO

Vishungi vya sigara vinaweza kudhuru maisha ya wanayama majini na kuharibu maji.
Unsplash/Brian Yurasits
Vishungi vya sigara vinaweza kudhuru maisha ya wanayama majini na kuharibu maji.

Iwajibisheni sekta ya tumbaku kwa uharibifu wa mazingira na afya ya binadamu:WHO

Afya

Ikiwa leo ni siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema sekta ya tumbaku inaathiri mazingira na afya ya watu na inahitaji kuwajibishwa zaidi kwa kusababisha uharibifu

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limefichua kwamba sekta ya tumbaku hugharimu dunia zaidi ya maisha ya watu milioni nane kila mwaka.

Pamoja na gharama kwa binadamu, miti milioni 600, ekari 200,000 za ardhi, tani bilioni 22 za maji, na tani milioni 84 za hewa ukaa au CO2 hutumiwa katika uzalishaji wa tumbaku.

Gharama nyingi za kimazingira huangukia katika nchi za kipato cha chini na cha kati, ambapo maji na mashamba hutumiwa kukuza mimea ya tumbaku, badala ya uzalishaji wa chakula, ambao mara nyingi unahitajika sana.

Ripoti ya WHO "Tumbaku: Kutia sumu kwenye sayari yetu" inatanabaisha kwamba kiwango cha hewa ukaa cha sekta hiyo kutokana na uzalishaji, usindikaji na usafirishaji wa tumbaku ni sawa na moja ya tano ya  hewa ukaa inayozalishwa na sekta ya ndege za kibiashara kila mwaka, na kuchangia zaidi katika ongezeko la joto duniani.

Matumizi ya tumbaku ni moja ya sababu kuu ya vifo vinavyoweza kuzuiwa.
Unsplash/Lex Guerra
Matumizi ya tumbaku ni moja ya sababu kuu ya vifo vinavyoweza kuzuiwa.

Matrilioni ya vichungi vinaichafua sayari dunia

"Bidhaa za tumbaku ni bidhaa zilizojaa zaidi kwenye sayari, zikiwa na zaidi ya kemikali 7,000 za sumu, ambazo huingia kwenye mazingira yetu zinapotupwa," amesema Dkt Ruediger Krech, mkurugenzi wa masuala ya kuchagiza afya katika shirika la WHO.

Ameongeza kuwa "Takriban vichungi vya sigara trilioni 4.5 huchafua bahari zetu, mito, barabara za mijini, mbuga, udongo na fukwe kila mwaka".

Bidhaa kama vile sigara, tumbaku isiyo na moshi na sigara za kielektroniki pia huongeza mkusanyiko wa uchafuzi wa plastiki.

Vichungi vya sigara vina bidhaa za plastiki na huvifanya kushika nafasi ya pili ya juu ya uchafuzi wa taka za plastiki ulimwenguni.

WHO inatoa wito kwa watunga sera kuvichukulia vichungi vya sigara sawa na plastiki yoyote ya matumizi ya mara moja, na kufikiria kuvipiga marufuku, ili kulinda afya ya umma na mazingira.

Licha ya sekta ya tumbaku, kutangaza soko la bodhaa hizo hakuna ushahidi uliothibitishwa kwamba vichungi vya sigara vina faida zozote za kiafya.

Wakulima wakitayarisha tumbaku tayari kuuza soko ya Mzingo, Malawi.
© FAO/Amos Gumulira
Wakulima wakitayarisha tumbaku tayari kuuza soko ya Mzingo, Malawi.

Walipisheni gharama wachafuzi

Gharama za kusafisha taka za bidhaa za tumbaku zilizozagaa huangukia kwa walipa kodi, badala yasekta inayoleta shida limesema shirika hilo la afya duniani.

Kila mwaka, hili linaigharimu China takriban dola bilioni $2.6 na India takriban dola milioni $766.

Gharama ya Brazil na Ujerumani ni zaidi ya dola milioni $200.

Lakini, nchi kama Ufaransa na Hispania na miji kama San Francisco, California nchini Marekani zinachukua msimamo.

Kwa kufuata kanuni ya “mchafuzi hulipa”, wametekeleza kwa ufanisi sheria ambayo inaifanya sekta ya tumbaku kuwajibika katika kuondoa uchafuzi inaousababish.

WHO inazitaka nchi na miji kuiga mfano huu, na pia kutoa msaada kwa wakulima wa tumbaku kubadili mwelekeo na kugeukia mazao endelevu, kutekeleza ulipaji ushuru mkubwa wa tumbaku na kutoa huduma za kusaidia watu kuacha matumizi ya tumbaku.

 

Siku ya kupinga matumizi ya tumbaku

WHO inaadhimisha siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani kila Mei 31. • Maadhimisho haya ya kila mwaka yanafahamisha umma juu ya hatari za kutumia tumbaku, hulka za biashara za makampuni ya tumbaku, WHO inafanya nini ili kupambana na janga la tumbaku, na kile ambacho watu ulimwenguni kote wanaweza kufanya ili kudai haki yao ya afya na maisha yenye afya bora na kulinda vizazi vijavyo. • Nchi Wanachama wa Shirika la WHO walitenga siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani mwaka 1987 ili kuitanabaisha dunia kuhusu janga la tumbaku na vifo vinavyoweza kuzuilika na magonjwa yanayosababishwa na tumbaku