Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika Kusini yaainisha madai ya vitendo vya mauaji ya kimbari ICJ dhidi ya Israel

Mahakama ya Kimataifa ya Haki yaanza kusikiliza kesi ya Afrika Kusini v. Israel huko The Hague.
ICJ-CIJ/ Frank van Beek
Mahakama ya Kimataifa ya Haki yaanza kusikiliza kesi ya Afrika Kusini v. Israel huko The Hague.

Afrika Kusini yaainisha madai ya vitendo vya mauaji ya kimbari ICJ dhidi ya Israel

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Leo Afrika Kusini imezungumza mbele ya mahakama ya Umoja wa Mataifa ya kimataifa ya haki ICJ baada ya kuwasilisha kesi katika jitihada za kukomesha mauaji ya raia huko Gaza, ikiishutumu Israel kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina madai ambayo Israel imekanusha vikali ikisema kuwa hayana msingi wowote

Hatua hii inafanyika wakati Gaza kwenyewe mashambulizi makubwa ya Israel kwa njia ya anga, ardhini na baharini yakiendelea kutwa kucha yakiwa yameathiri watu milioni 2.3, zaidi ya 23,000 kupoteza Maisha maelfu kujeruhiwa na zaidi ya milioni kutawanywa, Israel ikilipiza kisasi cha mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na Hamas tarehe 7 Oktoba ambayo yalisababisha vifo vya takriban raia 1,200 wa Israel na wa kigeni kusini mwa Israel na wengine 250 kuchukuliwa mateka.

Wakiwasilisha kesi yao, timu ya wanasheria wa Afrika Kusini wameiiambia ICJ mjini The Hague kwamba Israel imeonyesha "mfano wa mwenendo wa mauaji ya kimbari tangu ilipoanzisha vita kamili Gaza, eneo la kilomita za mraba 365 ambalo imekuwa ikilikalia  kimabavu tangu 1967.

Mahakama imeelezwa kuwa "Mauaji haya si kingine ila ni uharibifu wa maisha ya Wapalestina. Yanafanywa kwa makusudi, hakuna anayeachwa, hata watoto wachanga waliozaliwa”.

Wanachama wa timu ya wanasheria wanaowakilisha Afrika Kusini wanahudhuria kikao cha ICJ.
ICJ-CIJ/ Frank van Beek
Wanachama wa timu ya wanasheria wanaowakilisha Afrika Kusini wanahudhuria kikao cha ICJ.

Machafuko yasiyo na kifani

Hatua za Israel zimewafanya watu milioni 2.3 wa Gaza kukabiliwa na mashambulizi ya anga, nchi kavu na baharini ambayo hayajawahi kushuhudiwa, na kusababisha vifo vya maelfu ya raia na uharibifu wa makazi na miundombinu muhimu ya umma, amesisitiza Adila Hassim.

Israel pia ilikuwa imezuia msaada wa kutosha wa kibinadamu kuwafikia wale wanaohitaji na kusababisha hatari ya kifo kwa njaa na magonjwa kwa sababu ya kutowezekana kutoa msaada wakati mabomu yanaanguka, mwanasheria wa Afrika Kusini amedai.

"Wapalestina huko Gaza wanakabiliwa na mashambulizi ya mabomu popote wanapokwenda," Bi. Hassim ameiambia mahakama, akiongeza kuwa watu wengi wameuawa kiasi kwamba mara nyingi walizikwa bila kutambuliwa katika makaburi ya pamoja. 

Na wakati Wapalestina wengine 60,000 wamejeruhiwa na kulemazwa, amebainisha.

Hakuna palipo salama kwa Wapalestina

Ameendelea kusema kwamba Wapalestina wanauawa wakiwa majumbani mwao, katika maeneo wanayotafuta makazi, hospitalini, shuleni, misikitini makanisani na walipojaribu kutafuta chakula na maji kwa ajili ya familia zao. Pia wanauawa ikiwa wameshindwa kuhama katika maeneo ambayo wamekimbilia na hata kama walijaribu kukimbilia kwenye njia salama zilizotangazwa na Israel.”

Kama sehemu ya madai yake dhidi ya Israel, Afrika Kusini inadai kwamba mabomu 6,000 yalipiga Gaza katika wiki ya kwanza ya Israel kujibu mashambulizi ya Hamas. 

Hii ni pamoja na matumizi ya mabomu ya pauni 2,000 angalau mara 200 "katika maeneo ya kusini ya Ukanda huo ambayo yaliteuliwa kuwa salama, na kaskazini, ambapo kambi za wakimbizi zinapatikana” amesema Bi Hassim.

Silaha hizi zilikuwa "baadhi ya mabomu makubwa na ya uharibifu zaidi yanayopatikana", amesisitiza, akiongeza kwamba mauaji yakimbari hayatangazwi mapema, lakini mahakama hii ina faida ya wiki 13 zilizopita za ushahidi ambao unaonyesha bila shaka muundo wa tabia na uhusiano wa nia inayohalalisha madai yanayokubalika ya vitendo vya mauaji ya kimbari”.

Wajibu wa Mkataba

Ni kwa sababu ya hatua hizi ambapo Israel ilikiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, majaji wa ICJ baadaye walisikia, wakirejelea mkataba wa kimataifa uliotiwa wino na wanachama wa Umoja wa Mataifa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kuzuia uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mkataba huo "ulijitolea kuokoa ubinadamu", amesisitiza John Dugard, ambaye pia anawakilisha Afrika Kusini, na nchi zote ambazo zimetia saini Mkataba huo amesema "zina wajibu sio tu kuachana na vitendo vya mauaji ya kimbari bali pia kuyazuia", 

Kesi hiyo inaendelea Ijumaa kwa maelezo ya upande wa Israeli.