Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vizingiti vimetatiza uwasilishaji misaada kaskazini mwa Gaza

Mama akimtunza bmtoto wake msichanana katika Hospitali ya Nasser huko Khan Younis kusini mwa Gaza.
© UNICEF/Abed Zaqout
Mama akimtunza bmtoto wake msichanana katika Hospitali ya Nasser huko Khan Younis kusini mwa Gaza.

Vizingiti vimetatiza uwasilishaji misaada kaskazini mwa Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Wasaidizi wa kibinadamu wanatoa wito wa fursa ya ufikishaji misaada kwa haraka, salama, endelevu na usiozuiliwa kaskazini mwa Gaza kwani hali ya binadamu inazidi kuwa tete.

Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu wameshindwa kutoa msaada unaohitajika haraka wa kuokoa maisha kaskazini mwa Wadi Gaza kwa siku nne kutokana na ucheleweshaji na kukataliwa, pamoja na migogoro inayoendelea imeeleza Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura OCHA katika taarifa yake iliyokusanya takwimu za hadi jana Jan 4 na kuchapishwa leo Jan 5.  

Hii ni pamoja na dawa ambazo zingetoa msaada muhimu kwa zaidi ya watu 100,000 kwa siku 30, pamoja na lori nane za chakula kwa watu ambao kwa sasa wanakabiliwa na uhaba wa chakula unaohatarisha maisha.  

Watoto 

Kwa upande wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), linasema maelfu ya watoto tayari wamefariki dunia kutokana na ukatili huo unaoendelea, huku hali ya maisha kwa watoto ikiendelea kuzorota kwa kasi. 

"Watoto huko Gaza wanakumbwa na jinamizi ambalo linazidi kuwa baya kila kukicha," anasema Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa na shirika hilo leo mjini New York Marekani akiongeza kuwa, “Watoto na familia katika Ukanda wa Gaza wanaendelea kuuawa na kujeruhiwa katika mapigano, na maisha yao yanazidi kuwa hatarini kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika na ukosefu wa chakula na maji.” Anatoa wito kwamba watoto na raia wote lazima walindwe dhidi ya unyanyasaji na kupata huduma za kimsingi. 

Miundombinu ya afya 

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) linaeleza kamba tangu tarehe 24 Desemba 2023, limethibitisha mashambulizi manane kwenye hospitali ya Al-Amal, mashambulizi yaliyoua watu 7 na kujeruhi 11. Mashambulizi ya karibu zaidi ni ya jana Januari 4. 

Hospitali na miundombinu mingine muhimu ya matibabu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi imeshambuliwa karibu mara 600 tangu vita vilipozuka katika eneo hilo kujibu shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel, WHO imeeleza leo Ijumaa.

Mtandao wa WHO unaoangazia mashambulizi dhidi ya huduma za afya umeonesha mashambulizi 304 katika Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba. Mashambulizi hayo yaliathiri vituo 94 vya huduma za afya (pamoja na hospitali 26 zilizoharibiwa kati ya 36) na gari za wagonjwa 79.

Takriban watu 613 wamekufariki ndani ya vituo vya afya katika eneo linalokaliwa la Palestina tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana - 606 huko Gaza na saba katika Ukingo wa Magharibi - na zaidi ya 770 wamejeruhiwa, kulingana na takwimu za hivi karibuni za mashambulizi ya afya kutoka WHO

Wafanyakazi wa UN 

Pamoja na hali hii ngumu, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kusaidia watu katika kila hali inavyowezekana ijapokuwa ni katika hali hatarishi. Kufikia juzi tarehe 3 Januari, jumla ya wafanyakazi 142 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina (UNRWA) wameuawa tangu kuanza kwa mapigano hapo Oktoba 7.