Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Uvamizi wa Rafah itakuwa ni janga lisiloelezeka yaonya UN

Mavazi ya joto yanagawiwa kwa watu waliokimbia makazi yao huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Mavazi ya joto yanagawiwa kwa watu waliokimbia makazi yao huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Gaza: Uvamizi wa Rafah itakuwa ni janga lisiloelezeka yaonya UN

Amani na Usalama

Madaktari wa Umoja wa Mataifa leo wamesema wanahofia janga la kibinadamu lisiloelezeka endapo uvamizi kamili wa jeshi la Israeli utatokea Rafah kusini mwa Gaza ambako maelfu ya maelfu ya watu wamekimbilia tangu kuzuka kwa mzozo huu mpya Oktoba 7 mwaka jana. 

Likiunga mkono wasiwasi huo ulioelezwa pia na mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja na mkuu wa shirika la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, Mataifa Martin Griffiths kwamba kushambuliwa kwa Rafah "kunaweza kusababisha mauaji makubwa” Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO limesema kila liwezekanalo linapaswa kufanyika kuzuia mashambulizi hayo huku pia likikanusha vikali madai ya ushirikiano wa miaka mingi na washirika wasio wa afya ndani au chini ya hospitali za Gaza.

Hakuna ushirikiano

Dkt. Teresa Zakaria Msimamizi wa matukio wa WHO katika eneo linalokaliwa la Palestina amesema, "Hatuwezi kupaza sauti zaidi kukanusha kwamba hakuna ushirikiano kati ya WHO na taasisi nyingine yoyote isiyo katika sekta ya afya, washirika wa afya, na katika wizara ya afya ya Gaza ambao tunashirikiana nao," 

Naye Dkt. Rik Peeperkorn, Mwakilishi wa WHO katika eneo linalokaliwa la Palestina akizungumza kutoka Gaza amesisitiza kwamba hospitali "hazipaswi kuendeshwa kijeshi na kwamba macho yote sasa yako kwenye uhasama na mashambulizi makubwa yanayohofiwa huko Rafah. Unaona hofu inayowakabili watu. Na watu kila wakati huja na maswali wanauliza tunaweza kufanya nini?"

Maendeleo hayo yanakuja wakati vituo vya hospitali "vimelemewa na kutokuwa na uwezo  na viko ukingoni kusambaratika kabisa",amesema Dkt Peeperkorn huku akibainisha kuwa Wagaza milioni 1.5 sasa wamesongamana kwenye mahema ya muda na makazi ya UNRWA kila kona ya mkoa wa Rafah.

Mama akimtunza mwanawe na bintiye waliojeruhiwa katika shambulio la anga katika mji wa Gaza.
© UNICEF/Abed Zaqout
Mama akimtunza mwanawe na bintiye waliojeruhiwa katika shambulio la anga katika mji wa Gaza.

Hospitali zimezidiwa, zimefurika na vifaa havitoshi

Mganga huyo wa WHO amezitaja hospitali chache zilizosalia zinazofanya kazi kwa sehemu katika Rafah kuwa "zimezidiwa kabisa uwezo, zimefuroika na hazipatikani," akibainisha kuwa tangu Novemba, ni asilimia 30 tu ya operesheni za WHO kuelekea kaskazini ndizo zilizowezeshwa na mamlaka ya Israeli.

"Tangu Januari, idadi hiyo imekuwa ni ya chini zaidi operesheni imekataliwa au kuahirishwa," amesema Dkt. Peeperkorn akiongeza kuwa ni takriban asilimia 45 tu ya maombi ya operesheni ya kusini ndiyo yamewezeshwa. 

"Huo ni upuuzi, hata wakati hakuna usitishaji wa mapigano njia za kibinadamu zinapaswa kuwepo ili WHO, Umoja wa Mataifa na washirika wafanye kazi yao," amesema akiongeza kuwa "Tunahitaji mfumo kamili wa kuondoa migogoro ili kuweza kufanya kazi yetu. Umoja wa Mataifa na WHO, tuko tayari kutekeleza misheni zaidi na zaidi, kaskazini, katikati, na Kusini mwa Gaza.

Mauaji ya wanahabari yakome

Nao wataalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameonya juu ya athari mbaya za mzozo huo Gaza kwa maisha ya waandishi wa habari wakisema, "Tunasikitishwa na idadi kubwa ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari ambao wameuawa, kushambuliwa, kujeruhiwa na kuzuiliwa katika eneo la Palestina linalokaliwa hasa huko Gaza, katika miezi ya hivi karibuni wakipuuza waziwazi sheria za kimataifa. Tunalaani mauaji, vitisho na mashambulizi yote dhidi ya waandishi wa habari na tunatoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kuwalinda."