Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaonya, sasa Gaza imekuwa ukanda wa vifo

WHO iliongoza misheni mbili za kuokoa maisha kwa kuhamisha wagonjwa 32 walio katika hali mahututi, wakiwemo watoto 2, kutoka Nasser Medical Complex kusini mwa Gaza tarehe 18 na 19 Februari 2024 .
© WHO/Christopher Black
WHO iliongoza misheni mbili za kuokoa maisha kwa kuhamisha wagonjwa 32 walio katika hali mahututi, wakiwemo watoto 2, kutoka Nasser Medical Complex kusini mwa Gaza tarehe 18 na 19 Februari 2024 .

UN yaonya, sasa Gaza imekuwa ukanda wa vifo

Amani na Usalama

Hali mbaya ya kiafya na ya kibinadamu sasa imesambaa kote Gaza na inaendelea kuzorota, ameonya leo Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO. "Gaza imekuwa ukanda wa kifo," amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, akiwaambia waandishi wa habari katika mkutano huko Geneva Uswisi.

Ameongeza kuwa “Sehemu kubwa ya eneo hilo imeharibiwa. Zaidi ya watu 29,000 wamekufa na wengi zaidi wamepotea, wakidhaniwa wamekufa na wengine wengi zaidi wamejeruhiwa.” 

Katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita, utapiamlo umeongezeka kwa kasi tangu kuanza kwa vita tarehe 7 Oktoba, kutoka chini ya asilimia moja ya watu, hadi zaidi ya asilimia 15 katika baadhi ya maeneo.

Dkt. Tedros amesema "Idadi hii itaongezeka kadiri vita vitakavyoendelea na usambazaji wa misaada kukatizwa," huku akionyesha wasiwasi mkubwa kwamba mashirika kama vile la Mpango wa Chakula Duniani WFP hawawezi kufikia eneo la kaskazini mwa Gaza.

WFP ilisitisha utoaji wake wa misaada huko kutokana na ukosefu wa usalama kwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu na wale wanaotafuta msaada huo.

Tunaishi dunia gani

"Tunaishi dunia ya aina gani wakati watu hawawezi kupata chakula na maji, na wakati watu ambao hawawezi hata kutembea hawawezi kupata huduma?", almejoji mkuu huyo wa WHO na kuendelea kusema kwamba "Tunaishi katika ulimwengu wa aina gani wakati wafanyakazi wa afya wako katika hatari ya kushambuliwa kwa mabomu wanapofanya kazi yao ya kuokoa maisha na hospitali zinalazimika kuungwa kwa sababu hakuna nishati au dawa tena za kusaidia kuokoa wagonjwa?"

Amesisitiza hitaji la usitishaji mapigano mara moja, mateka kuachiliwa, bunduki kunyamaza, na fursa ya ufikiaji wa wanaohitaji msaada wa kibinadamu usio na kizuizi.

"Ubinadamu lazima ushinde," amesisitiza Dkt. Tedros.

Watu kuhamishwa hospitali

Katika muda wa siku tatu zilizopita WHO na washirika wake wamefanya operesheni kadhaa za dharura kwenye kituo cha matibabu cha Nasser huko Khan Younis, kusini mwa Gaza, ili kuwahamisha wagonjwa mahututi, wakiwemo watoto.

"Kwa kuwa vitengo vya wagonjwa mahututi havifanyi kazi tena, WHO imesaidia kuhamisha wagonjwa, ambao wengi wao hawawezi hata kutembea," amesema Tedros.

Karibu wagonjwa 130, watu waliojeruhiwa na angalau madaktari na wauguzi 15 wamesalia hospitalini hapo, huku kukiwa na operesheni zinazoendelea za jeshi la Israeli, hakuna umeme na maji ya bomba hayatoki na kuna upungufu mkubwa wa vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha.