Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila MONUSCO ningalikuwa bado msituni – Mpiganaji wa zamani DRC

Mwanamke akiwa amebeba mwanaye mgongoni akielekea nyumbani katika jimbo la Kivu Kaskazini DRC. (Kutoka maktaba)
OCHA/Ivo Brandau
Mwanamke akiwa amebeba mwanaye mgongoni akielekea nyumbani katika jimbo la Kivu Kaskazini DRC. (Kutoka maktaba)

Bila MONUSCO ningalikuwa bado msituni – Mpiganaji wa zamani DRC

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kazi ya kuhesabu kura za Rais kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 20 na kuendelea katika maeneo mengine siku zilizofuata, inaendelea huku nao wanufaka wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO ambao umeanza kufunga virago, wakitoa shukrani zao.

Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini DRC, CENI, inaendelea kutangaza matokeo ya Urais halikadhalika matokeo ya magavana, wabunge na madiwani, huku mshindi wa kiti cha Urais akitarajiwa kutangazwa tarehe 31 mwezi huu wa Desemba. 

Kwingineko nchini humo hususan jimboni Kivu Kaskazini, MONUSCO inaanza kufunga ofisi zake kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia ombi la serikali. 

Ofisi ya hivi karibuni zaidi kufungwa ni ile ya Lubero jimboni humo ambako Gentil Kakule Kombi alishukuru uwepo wa MONUSCO kwenye eneo hilo kwa miaka 21. 

Amesema ni kwa msaada wa MONUSCO nilitoka porini, nikasalimisha silaha na sasa nimetulia vema kabisa kwenye jamii yangu na ninashikiri kwenye harkati za ujenzi wa amani.” 

Anakumbuka MONUSCO kumpokea Rutshuru na kisha kusafirishwa kwa basi na kukabidhiwa kwa serikali ambako walipatiwa program ya kujumuishwa tena kwenye jamii. 

Gentil alijisalimisha mwaka 2015 na sasa ni mwanachama wa klabu ya soka ya Lubero inayocheza kwenye ligi ya jimbo la Kivu Kaskazini.